Utafiti: Utumiaji wa Facebook kupita kiasi huhamisha usaliti wa mapenzi

Mtandao wa facebook ambao ulianzishwa kama utani miaka 10 iliyopita (February 4, 2004) na mwanafunzi wa chuo kikuu cha Harvard, Mark Zuckerberg, imekuwa ni njia rahisi ya kuwasiliana ambayo imeunganisha dunia na kuwaongezea watu marafiki wapya, huku ikiwarudisha pamoja walipotezana.




Ukiacha mbali faida kubwa inayotokana na utumiaji wa facebook, faida ambazo ukizitaja unaweza kujaza kitabu kikubwa bila kuzimaliza huku zikiongozwa na faida moja kubwa ‘Kuunganisha Watu kirahisi’, zipo hasara kubwa ambazo zinatokana na utumiaji wa mtandao huu kupita kiasi.

Utafiti uliofanywa na Rusell B. Clayton, Alexander Nagurney na Jessica R. Smith, na kuchapishwa kwenye Journal ya ‘Cyberpsychology, Behaviour and Social Networking’, umebaini kuwa utumiaji wa Facebook kupita kiasi humjengea mtumiaji tabia/hali ya kutokuwa muaminifu katika mahusiano ya mapenzi.

Katika utafiti huo, Dr. Ramadhani Rursavasula, mtaalam wa saikolojia na mahusiano, ameeleza kuwa watu wengi wameigeuza facebook kuwa mbadala au sehemu ya kukimbilia kutoka kwenye mahusiano yao ya ukweli, na mwisho huishia kudanganya na kusaliti wapenzi wao kwa kuanzisha mahusiano ya siri na wapenzi wao wa zamani ama watu waliokuwa na mahusiano ya kawaida hapo awali.

Katika utafiti huo ambao ulijikita zaidi katika mahusiano yaliyodumu kwa muda wa chini ya miaka 3, ulibaini kuwa mtandao wa Facebook pia unaweza kusababisha watu walio katika mahusiano kuwa na hali ya kutoaminiana kwa kiasi kikubwa na kukosa amani katika mapenzi yao.

Matokeo ya utafiti huu unaungana na mfano wa habari iliyowahi kuchapishwa kwenye mtandao wa CNN, July 6, 2010.

Mtandao huo ulichapisha habari kuwa, Ken Savage (38), alikuwa na mkewe aliyekuwa ametoka kwenye uathirika na msongo wa mawazo na matumizi ya dawa za kulevya, hivyo akaona ni vyema kumtafutia kitu cha kumpa kampani hususani rafiki zake wa zamani. Hivyo akamuunganisha na mtandao wa Facebook.

Lakini ghafla, Ken alianza kumuona mkewe akiwa anaficha screen ya computer pale jamaa anapoingia ghafla chumbani kwake. Mwishoni akagundua tayari alikuwa ameanza kutumia mtandao huo kuwasiliana mpenzi wake wa zamani.

Mbali na utafiti huo pale juu na mfano huo, miaka mitatu iliyopita kuna utafiti mwingine uliofanywa nchini Marekana na kundi la wanasheria (The American Academy of Matrimonial Lawyers).

Utafiti huo uliojikita katika mahusiano kati ya wana ndoa wanasheria (Attorneys), ulibaini kuwepo kwa ongezeko la kesi za kudai talaka kwa asilimia 81, zinazotumia mtandao wa kijamii hususani Facebook kama ushahidi wa usaliti uliofanywa na wenzi wao.

Utafiti mwingine uliofanywa na mtandao wa Divorcce-Online wa Uingereza, uliozipitia zaidi ya kesi 5,000 za madai ya talaka, na uligundua kuwa Facebook ilitajwa kwa asilimia 20 kama sababu ama kilelezo cha ushahidi wa usaliti wa wenzi wao.

Hata hivyo, mtandao huu umeweza pia kuzirudisha ndoa zilizokuwa zimevurugika kutokana na usaliti japo ni kwa kiasi kidogo na muda mwingine kiutani.

Kwa mfano, September mwaka jana, ndoa ya Ivan Lewis na Sonya Gore ilikuwa mashakani baada ya Ivan kumsaliti Sonya, na kupelekea wawili hao kutengana kwa miezi 10.

Lakini, Ivan aliamua kuandika kwenye karatasi kwa mkono wake na kupost picha hiyo kwenye facebook ikiwa na maandishi yanayokiri kuwa alimsaliti mkewe (I cheated on my wife!!!).

Mkewe alipoona hiyo post, alimwambia Lewis kuwa kama post hiyo ikipata likes 10,000 tu atamsamehe na kumrudia. Kwa bahati nzuri ilipata zaidi ya Likes 15,000, hivyo Likes za facebook zikaiokoa ndoa hiyo.

Kama wewe ni mtumiaji wa Facebook kupitiliza, kuwa makini na matumizi yako na uhusiano wako, isije kuwa sababu ya kukushawishi kusaliti kwa kuwa wamiliki wa mtandao huo hawahusiki na faida wala hasara utakazozipata kwenye mahusiano yako kupitia Facebook.

Msemaji wa Facebook, Andrew Noyes, aliwahi kusema kuwa mtandao huo hauhusiki kivyovyote na uharibifu wa ndoa unaojitokeza..

Siku Njema..!
Previous Post Next Post