ZUMA AZINDUA SANAMU YA NELSON MANDELA....

Pretoria, Afrika Kusini. Rais Jacob Zuma amezindua sanamu ya shaba ya shujaa wa Afrika, Nelson Mandela kwenye jengo la Muungano lililopo mji wa Pretoria.
Sanamu hiyo yenye urefu wa mita tisa humuonyesha Mandela akitabasamu, huku akiwa ameonyesha ishara ya kukumbatia.



Wakati akizindua sanamu hiyo jana, Rais Zuma alisema kwamba sanamu nyingi za Mandela zinamuonyesha akinyoosha mkono wake mmoja juu kama ishara ya mapambano iliyokuwa ikitumiwa na Chama cha ANC.

Lakini, ishara ya kukumbatia iliyokuwa ikitumika katika sanamu hii ni tofauti, kwasababu inamuonyesha Madiba akikumbatia nchi nzima na watu wake wote bila kujali rangi, itikadi wala tabaka. Zuma aliizindua sanamu hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mazishi ya kiongozi huyo yaliyoshuhudiwa na umati mkubwa watu mbalimbali, wakiwamo viongozi wa nchi tofauti yaliyofanyika katika Kijiji cha Qunu.

Katika uzinduzi huo alikuwapo Waziri wa Utamaduni, Paul Mashatile na familia ya Madiba ambapo Zuma alikuwa na mkewe, Thobeka Madiba Zuma.

Pia, alikuwapo Makamu wa Rais, Kgalema Motlanthe na viongozi wengine nchini humo wakishuhudia kuzinduliwa kwa sanamu hiyo ya historia.

Uzinduzi huo uliofanyika katika jengo hilo, pia ulishuhudiwa na waandishi wa habari kutoka sehemu mbalimbali.

Mandela alizikwa juzi katika kijiji ambacho alizaliwa cha Qunu, mazishi yake yalihudhuriwa na umati mkubwa wa watu wakiwamo viongozi mbalimbali duniani.


Source: Mwananchi 
Previous Post Next Post