Barua ya wazi kwa Sitti Abbas Mtemvu, Miss Tanzania 2014

Mpendwa Sitti Abbas Mtemvu-Miss Tanzania 2014

Ni matumaini yangu umzima wa afya, na kila Mtanzania angependa kukuona katika hali hiyo.

Binafsi si Mpenzi wa mashindano ya U-Miss nchini, lakini kuna jambo linalonihusu kama raia wa kawaida anayejivunia utaifa wake. Mimi ni Mtanzania kama ulivyo wewe na walivyo wengine.

Kwenye utaifa kuna kitu kinaitwa “Allegiance” kwa kamusi ya Oxford, maana yake ni “the act of binding yourself (interlectually or emotionally) to a course of action” au “loyalty that citizens owe to their country (or subjects to their sovereign)”.



Kwa tafisiri isiyo rasmi ya neno “Allegiance” ni utiifu anaopaswa kuwa nao raia dhidi ya taifa lake pale anapojitolea kufanya jambo kwa ajili ya taifa lake, au kiapo ambacho mtu hukichukua kuahidi kuwa atatimiza jukumu alilopewa.

Hivyo basi, endapo utakwenda kinyume na ulichokiapia, basi huna budi kuubeba mzigo.

Siamini kuwa lilikuwa ni lengo la kutaka “Umaarufu” ndilo lililokusukuma kuwania taji hilo, bali ni upendo kwa jamii yako, Watanzania na hata kwa bara la Afrika kijumla, lakini kama hilo ndilo lilikuwa moyoni, kwanini umetumia njia batili kutaka kufanya mazuri.

Naweza kufafanisha na bondia, kila mpiganaji, lengo na furaha yake ni kutwaa taji, lakini si vema akainyemelea heshima hiyo kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu, si sahihi dada yangu.

Uongo ni utumwa, ukweli ni uhuru (ukombozi), kudanganya si jambo aula, kwa sababu tangu sakata hili liingie vichwani na vinywani mwa waandishi wa habari ni dhahiri linakukera, linakuumiza moyo wako kwa sababu kiasili si jambo linalojenga, uongo huharibu wajihi na taswira ya mtu, na kila mtu atatumia fimbo hiyo kukuchapa.

Hebu watendee haki Watanzania, kivipi? Kumbuka si kila mtu anayekuandama hakupendi, bali wanataka uhalali wako, hawamtaki Fake and Cheap Sitti Abbas Mtemvu, na hata kama haufudhu huko haimaanishi kuwa Sitti hawezi kuishi bila hilo taji. Wajibika tafadhali. Kama ni kweli haukustahili, milango ipo mingi, unapong’ang’ania hilo unazidi kuuvua utu wako.

Jambo jingine ni mahojiano na waandishi wa habari, watu wasingekujua bila mchango wa waandishi wa habari, wala wasingetambua kuwa ni binti wa Mbunge wa Temeke, aliyekuwa anaishi Texas, Marekani, ila kupitia hao watumishi wa jamii (waandishi wa habari), wengi wamekutambua, hivyo basi waheshimu, wakikuuliza maswali wajibu, ukijibu ‘nyodo’ unazidi kuwaangusha mashabiki wako.

Tangu Oktoba 11 ulipokabidhiwa taji, kumbuka ulishatoka kuwa Ms Sitti Abbas Mtemvu na kuwa Miss Tanzania Sitti Abbas Mtemvu, hayo majina mawili ya kwanza (Miss Tz) yana maana na dhima kubwa zaidi ya unavyofikiria, kuna wasichana wangapi wanataka kuipeperusha bendera ya taifa lao? Tatizo si kuibeba bendera, suala unastahili kuipewa?

Njia za mkato hazina heshima, mwaka 1974, Hellen Elizabeth Morgan alichaguliwa kuwa Mrembo wa Dunia, siku nne baadae raia huyo Uingereza alirudisha taji hilo baada ya kugundulika kuwa alikuwa na mtoto, hivyo basi wadhifa huo akapewa mshindi wa pili Annelina Kriel kutoka Afrika Kusini.

Wewe si wa kwanza kukumbwa na dhahama hiyo lakini ukiwa mtiifu na kuwajibika utakuwa mfano kwa washiriki wengine watakaofuatia kujua wajibu, ukubwa na heshima ya mashindano na taji hilo.

Tunahitaji Balozi mkweli na mtiifu ambaye hatouza taifa lake kwa hayawani.

Editor
Previous Post Next Post

Popular Items

EXPENSIVE THING OF THE DAY

New Music: Blue - Pesa