KOPLO ADAIWA KUTAPELI SH MILIONI 45


ASKARI polisi mmoja mwenye cheo cha koplo, anashikiliwa mahabusu katika Chuo cha polisi Moshi kwa tuhuma za kutapeli Sh45 milioni kutoka kwa vijana 154 aliowaahidi angewapatia ajira Polisi.
Mbali na kushikiliwa kwa polisi huyo, ofisa mwenye cheo cha Kamshina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), amesimamishwa kazi kwa madai ya kuhusika na mtandao huo wa utapeli.
Imebainika kuwa ofisa huyo alitapeli vijana 154 wa kidato cha nne na sita kuwa angewawezesha kujiunga na Jeshi la Polisi hivyo kujikusanyia Sh700,000 na Sh900,000.
Habari za uhakika kutoka makao makuu ya polisi jijini, zimeeleza koplo huyo aliamriwa na wakuu wake wa kazi kwenda kujisalimisha mwenyewe Chuo cha polisi Moshi zamani kikijulikana kama CCP.
“Tarehe 6.2.2013 ndiyo aliripoti kwa mkuu wa chuo kule Moshi na kuwekwa mahabusu akisubiri kufunguliwa mashtaka ya kijeshi,”amedokeza Ofisa mmoja makao makuu ya polisi Dar.
Habari hizo zimedai Oktoba 13,2012, Ofisa huyo wa Polisi alighushi saini ya Ofisa wa Utawala makao makuu ya polisi, Thobias Andengenye na kutuma simu ya upepo CCP ikiwa na majina ya vijana hao.
Simu hiyo iliyotumwa kwa Commandant Moshi Police Academy ikimwagiza mkuu wa chuo hicho cha Polisi awapokee vijana hao 154 kwa kuwa usajili wao umekamilika hivyo waingie chuoni.
Simu hiyo ambayo gazeti hili limefanikiwa kuiona, inaendelea kusomeka kuwa” Wapokee ili waungane na wenzao kwa usajili wa chuo ili waendelee na mafunzo ya awali ya askari polisi”.
Taarifa zaidi zinadai kuwa simu hiyo iliyokuwa na sahihi ya T.B. Andengenye (SACP), haikutumwa moja kwa moja CCP bali ilipitia Polisi Moshi na kupelekwa kwa mkono chuoni.
Baada ya siri kifichuka, Polisi makao makuu Dar es Salaam walimwita koplo huyo na kumuamuru aende mwenyewe CCP Moshi ambako aliripoti juzi na kuwekwa mahabusu.
Juhudi za kumpata Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso ili kufafanua juu ya suala hilo ziligonga mwamba baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
Hata hivyo, mmoja wa maofosa waandamizi makao makuu Dar es Salaam, alisema suala hilo kwa sasa linafanyiwa kazi kwa taratibu za kijeshi na kwamba hatua zaidi za kiraia kama vile kumfikisha mahakamani zinaweza kufanyika baadae.
Source: Mwanachi

Previous Post Next Post