JOHN MNYIKA ASEMA: SHERIA MPYA ZINAWALINDA MAFISADI

Mbunge wa Jimbo la Ubungo akichangia jambo Bungeni

MBUNGE wa Ubungo Jijini Dar es Salaam (Chadema), John Mnyika amemtaka, Rais Jakaya Kikwete kutosaini marekebisho ya sheria mpya ya mabadiliko katika Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008.
Mnyika pia anakusudia kukata rufaa juu ya uamuzi wa Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa kutumia vibaya kanuni za Bunge kutokana na kitendo chake cha kuzivunja kamati tatu za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Serikali Kuu (PAC).
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, jana, Mnyika alisema Rais Kikwete kabla ya kusaini marekebisho hayo ambayo yanaonyesha dalili za kuwalinda mafisadi, ajitokeze na kuwaeleza Watanzania faida na hasara ya mabadiliko ya sheria hiyo.
Wiki hii Serikali iliwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko katika Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008, huku ikiongeza vifungu ambavyo vinapunguza nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Marekebisho hayo yamo kwenye Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria, namba tatu wa mwaka 2012 uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Marekebisho hayo yanapendekeza kubadili utaratibu mzima wa kushughulikia taarifa hiyo, kwani yanaongeza vipengele, vinavyoliwajibisha Bunge kwa Serikali.
Serikali imeongeza vipengele vya ziada ambavyo vinazitaka kamati za Bunge zinapofanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, kupeleka maazimio yake kwa Serikali ili yatafutiwe majawabu badala ya utaratibu wa sasa wa kupeleka hesabu zake bungeni.
Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini alisema marekebisho hayo hayana tija kwa taifa ambalo linapigania kuwakomboa wananchi huku likiacha mianya ya wajanja kuendelea kutumia mali za umma bila kuchukuliwa hatua.
“Rais ndiye mwenye uamuzi wa mwisho hivyo anatakiwa kutambua kuwa marekebisho hayo ambayo yako mikononi mwake hapaswi kuyasaini hadi pale atakapowaeleza ukweli wananchi nia ya mabadiliko ya sheria hiyo,” alisema Mnyika.
Mnyika amesema amemwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila akimtaka kumpatia mtiririko wa uamuzi wa Spika Makinda wakati alipotangaza kuvunja kamati tatu za Bunge ili aweze kukata rufaa.
Alisema amekuwa akitaka kufanyika kwa mabadiliko ya kanuni ya Bunge ya 152 (3) inayompa mamlaka Spika kuchukua uamuzi peke yake pasipo kushirikiana na mtu mwingine.
“Spika Makinda amezivunja kamati tatu kwa kutumia kanuni ya Bunge 152 (3), wakati huo huo licha ya kwamba amezivunja lakini bado zinatambulika katika kaununi hiyo hiyo ya Bunge ya 114 (11). Sasa sijui Spika ameliona hili au la,” alisema Mnyika.
Alisema atatumia sheria za kanuni za Bunge 5 (4) inayompata uhuru Mbunge kukata rufaa kama hajaridhika na uamuzi wa Spika ili hatua zaidi zichukuliwe.
Juzi Spika Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati za kudumu za Bunge, huku Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kufutwa.
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitaendelea kufanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo itaendelea na jukumu lake la msingi la kuchambua taarifa ya CAG pia kwa Serikaki Kuu.
Source: Mwananchi
Previous Post Next Post