Mtanzania anahitaji shilingi 869 kwa siku?

Imebainika kuwa kila Mtanzania anahitaji sh 869.5 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya chakula kila siku ikilinganishwa na sh 414.8 mwaka 2007.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya Salum, wakati wa uzinduzi wa chapisho la utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi wa mwaka 2011/12, uliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Alisema utafiti huo unaonesha sh. 26,085 zilihitajika mwaka 2011/12 ili kukidhi mahitaji ya kununua chakula kwa mtu mzima mmoja kwa mwezi, ambazo ni sawa na sh 869.5 kwa siku ikilinganishwa na sh 12,444 sawa na sh 414.8 kwa siku mwaka 2007.



Mkuya, pia alisema kiasi sh 36,482 kinahitajika kukidhi mahitaji ya msingi ya mtu mzima mmoja kwa mwezi, ikilinganishwa na sh 19,201, sawa na mahitaji ya aina hiyo mwaka 2007.

Alisema kutokana na chapisho hilo, inaonyesha kuwa mwenendo wa hali ya umasikini nchini umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2011/12.

“Baadhi ya taarifa muhimu zilizomo katika chapisho hili ni pamoja na taarifa za mapato, matumizi na manunuzi ya kaya, elimu, afya, shughuli za kiuchumi na ajira,” alisema Mkuya.

Aidha, alisema umasikini kwa wakazi wa maeneo ya vijijini bado ni changamoto kubwa ikilinganishwa na wakazi wanaoishi mijini.

“Utafiti unaonesha kuwa kwa kila watu 100 waliokuwa na uwezo wa kufanya kazi mwaka 2011/12, watu 75 walijishughulisha na kilimo na uvuvi.

“Hata hivyo, matumizi ya zana duni za kilimo bado ni changamoto kubwa inayoendelea kutukabili, kwani utafiti unaonesha kuwa asilimia 96.5 ya kaya zinazojishughulisha na kilimo zinatumia jembe la mkono,” alisema Mkuya.

Aliongeza kuwa ni asilimia 0.1 ya kaya ndio zinazotumia zana za kisasa za kilimo, likiwemo jembe la plau na trekta.

Akizungumzia upande wa afya, Mkuya alisema utafiti umeonesha kwamba, idadi ya watu waliopata huduma za afya katika hospitali na zahanati za serikali imeongezeka kutoka asilimia 41.6 mwaka 2007 hadi asilimia 55 mwaka 2011/12.

Naye Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndullu, alishangazwa na kasi ya kupungua umasikini katika Jiji la Dar es Salaam kutoka asilimia 14 hadi nne katika miaka mitano, hiyo ni kasi kubwa, lakini kwenye miji mingine kasi haiko hivyo.

Alisema pamoja na umasiki kupungua, lakini la kujifunza ni kwamba umasikini katika maeneo ya vijijini bado ni mkubwa, hivyo ni vema nguvu zikaelekezwa huko.

Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB), Philipe Dongier, alisema pamoja na ripoti hiyo kuonesha matumaini, bado kuna haja ya kuifanyia kazi kwa sababu bado ziko kaya ambazo haziwezi kula zaidi ya mlo mmoja kwa kwa siku.

Chanzo: Tanzania Daima
Previous Post Next Post

Popular Items

EXPENSIVE THING OF THE DAY

New Music: Blue - Pesa