Millen Magese: Mwanamke jasiri aliyejitangaza mgumba kuwapa moyo wanawake wengine wenye tatizo hilo

Kwa kila mwanamke aliyekamilika, jambo la muhimu katika maisha yake duniani, ni kuzaa mtoto/watoto. Mungu alimuumba mwanamke kutoka kwenye ubavu wa mwanaume, si tu kuwa msaidizi wake, bali kuwa nusu ya pili ya uumbaji wa mtoto kupitia mimba kutoka kwa mbegu za mwanaume.


Ndoa nyingi zinazofungwa kwa gharama kubwa, ya kawaida ama ndogo, haziwezi kuwa na furaha iliyokamilika kama haitopata mtoto/watoto. Na mtu anayenyooshewa kidole zaidi katika ndoa isiyokuwa na watoto ni mwanamke kwakuwa tatizo la kutozaa pamoja na kuwaathiri pia wanaume, lipo kwa kiasi kikubwa kwa wanawake.

Hivyo mwanamke anapokuwa mgumba, huishi kwa maisha ya huzuni na majonzi makubwa. Hujiona ni mtu mwenye kasoro na mara nyingi ndugu wa mwanaume humwangalia kwa jicho la baya. Mwanamke huyo huishia kuhangaika katika hospitali, waganga wa kienjeji ama kuombewa kanisani ili kujaribu kuondoa tatizo hilo. Sio wote wanaofanikiwa kwakuwa wengine ugumba wao hauwezi kutibika. Kwa wenye tatizo la Endometriosis, tatizo linalosababishwa na seli za tumbo la uzazi kuwa nje ya kizazi, ugumba ni tatizo kuu.

Wapo wanawake wengi wenye tatizo lakini ni wachache wenye ujasiri wa kujitokeza hadharani kusema. Miss Tanzania wa zamani na mwanamitindo wa kimataifa aliyehamishia makazi yake nchini Marekani, Happiness Millen Magese ni mmoja wa watu hao wachache.



Millen ameamua kujitokeza kwa ujasiri mkubwa na kuanzisha kampeni ya kukuza uelewa juu ya tatizo hilo. Ukikutana na Millen, utagundua kuwa ni msichana mrembo, mcheshi na anayetabasamu mara nyingi. Huwezi kujua ni kwa kiasi gani tatizo hilo limemtesa kiasi cha kufanyiwa upasuaji mara 12 katika maisha yake.

“Nikiwa sekondari nilikuwa napatwa na ugonjwa ambao kwa wakati huo niliona ni wa kawaida.Nilikuwa napata maumivu makali wakati wa hedhi yaliyonisababishia kutapika na wakati mwingine kupoteza fahamu,” Millen aliiambia Clouds TV.

“Kila nilipoingia kwenye hedhi nililazimika kulazwa kwa siku sita hadi kumi hospitalini,kutokana na maumivu hayo kuna wakati wanafunzi wenzangu waliwahi kunihoji ni kwa nini mimi kila mwezi lazima niugue Niliteseka sana, nakumbuka kuna siku nilizidiwa wakati mama yangu hayupo.Baba akachukua jukumu la kunibeba na kunipeleka hospitali.

Nilipokuwa kwenye maumivu makali aliniambia nijikaze kama mwanamke, hivyo nikawa namficha baba maradhi yangu, ingawa ilikuwa kila mwezi kama siyo kunipeleka hospitali yeye basi lazima aje kunitazama hospitali.”

Millen alisema hata baada ya kujiingiza kwenye masuala ya urembo, bado hali ya maumivu wakati wa hedhi iliendelea.

“Nikiwa hapa nyumbani sikujua nasumbuliwa na nini. Siku moja nikaamua kwenda kupima wakati huo nikiwa Afrika Kusini, nikagundulika kuwa na ugonjwa wa Endometriosis na tiba pekee ikawa kufanyiwa upasuaji,” alisema.

Huko alifanyiwa upasuaji mara ya kwanza na kuonyesha yai lake moja ni bovu hivyo kutakiwa litolewe ingawa alikuwa na uwezo wa kubeba mimba. “Nilifanyiwa upasuaji mara ya pili,kila siku nikalazimika kuwa nafanyiwa uchunguzi ili kubaini maendeleo ya hali yangu, lakini cha kushangaza hali ilizidi kuwa mbaya.Kuna wakati nilijiuliza kwa nini mimi?



Millen anasema ameshafanyiwa upasuaji mara 12 hadi sasa
Alisema katika kipindi hicho alikuwa anachoma sindano kila asubuhi kwa siku 63 ili kunusuru kizazi chake bila mafanikio, aliendelea kufanyiwa upasuaji mara 12 zaidi. Kwa sasa Magese hana uwezo tena wa kushika mimba lakini hajakataa tamaa. Ameamua kuanzisha kampeni hiyo kuwasaidia wanawake wengine wenye tatizo hilo.

Tayari ameshaanza kupata misaada kutoka kwa watu mbalimbali wa Marekani kama vile taasisi ya Swan Development LLC, Texas ambao wameahidi kumpatia mashine za za kutambua tatizo na upasuaji pamoja na dawa, ambapo angependa ziwekwe hospital ya Dar es salaam kulingana na mapendekezo ya wadau ingawa lengo lake la muda mrefu ni kufungua hospital itakayojihusisha na magonjwa ya wanawake na ndio maana anaomba msaada wa serikali na wananchi kwa ujumla ili kufanikisha lengo hilo.



Millen na wasichana mbalimbali kwenye kampeni kuhusu tatizo hilo

Magese anawataka watoto kuwaambia wazazi pindi wanapokuwa wakipatwa na maumivu makali yaliyopitiliza wakati wakiwa kwenye siku zao za hezi na pia wazazi kujadiliana na watoto wao punde hali hiyo inapotokea na kuwawahisha hospital ili wapatiwe huduma sahihi.
Previous Post Next Post