PICHA: RAISI JAKAYA KIKWETE AFUNGUA RASMI UJENZI WA BARABARA YA BWANGA - BIHARAMULO



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (aliyeshika mkasi) akikata utepe kuzindua rasmi ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo. Kushoto kwa Rais ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John P. Magufuli na kulia kwa Rais ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Alhaj Eng. Mussa Iyombe. Wengine katika picha ni baadhi ya Mawaziri, Wabunge na Viongozi wa Mikoa ya Geita na Kagera walioshiriki katika sherehe hizo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipanda mti katika eneo la Buziku mkoani Geita wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo.


Umati wa wananchi waliojitokeza kumlaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipowasili eneo la Buziku mkoani Geita tayari kwa uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo.(P.T)


JK Amkabizi Magufuli Majukumu Mazito

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtaka Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kuhakikisha kuwa Sheria ya Usalama Barabarani inasimamiwa vizuri ili kuhakikisha kuwa barabara zinazojengwa nchini zinadumu kwa muda uliokusudiwa.

Akizungumza katika eneo la Buziku mkoani Geita wakati akizindua ujenzi wa barabara ya Bwanga hadi Biharamulo yenye urefu wa kilometa 67, Rais Kikwete alisema kuwa wizara ya Ujenzi ni lazima ihakikishe inasimamia sheria zilizopo na hasa hii ya kutoruhusu magari yenye uzito uliozidi viwango vilivyoainishwa katika Sheria Namba 30 ya Mwaka 1973.

Akisistiza umuhimu wa kutunza barabara Rais Kikwete alibainisha kuwa "adui wakuu watatu wanao sababisha barabara kuharibika mapema ni; magari yanayobeba mizigo zaidi ya uzito uliowekwa kisheria, ujenzi duni usiozingatia viwango na kuachwa kwa maji kuzagaa barabarani".

Wakati huo huo Rais Kikwete alielezea kufurahishwa kwa kuanza ujenzi wa mradi huo kwani wapo baadhi ya watu waliokuwa waliokuwa wakieneza taarifa kuwa sehemu hiyo ya barabara haiwezi kujengwa lakini sasa wameumbuka.

Awali akitoa maelezo ya mradi huo Mtendaji Mkuu wa Tanroads Injinia Patrick Mfugale alielezea kuwa mradi mradi wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umegharimu Shilingi bilioni 55 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania. "Mradi huu utajengwa kwa muda wa miezi 27 na hivyo kukamilika mwezi Februari mwaka 2015" alisema Injinia Mfugale.

Naye Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Magufuli alimhakikishia Rais Kikwete kuwa wizara yake itahakikisha kuwa inamsimamia mjenzi wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya Sinohydro Ltd. ya kutoka Jamhuri ya Watu wa China ili aukamilishe kwa muda na viwango vilivyokusudiwa na bila ya visingizio vya nyongeza ya gharama.

Akimpongeza Rais kwa kutekeleza ahadi yake, Waziri Magufuli alibainisha kuwa wananchi wa mikoa ya Geita na Kagera wamefurahishwa sana kuona kuwa hatimaye barabara hiyo muhimu inajengwa kwani hiyo ndiyo sehemu pekee iliyokuwa imebaki ikiwa haina lami kwa barabara inayounganisha mikoa hiyo ya ziwa.

Previous Post Next Post