TFDA KUWAENDELEZA WAJASIRIAMALI WA CHAKULA



 Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Bi. Gaudensia Simwanza KUSHOTO akieleza kwa waandishi wa Habari kuhusu mpango wa mafunzo na Ufuatiliaji kwa wazalishaji wadogo wa bidhaa za Chakula unaoratibiwa na mamlaka hiyo, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo Jijini Dar es Salaam KULIA ni Mkaguzi wa Chakula toka Mamlaka Hiyo Bw. John Mwingira.
Mkaguzi wa Chakula toka Mamlaka ya Chakula na Dawa Bw. John Mwingira akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mpango wa ukaguzi wa vyakula kutoka kwa wazalishaji, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo Jijini Dar es Salaam KULIA ni Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo Bi. Gaudensia Simwanza

PICHA NA HASSAN SILAYO> MAELEZO
========  ========  =========


MAELEZO KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MPANGO WA MAFUNZO NA UFUATILIAJI KWA WAZALISHAJI WADOGO WA BIDHAA ZA CHAKULA , UKUMBI WA IDARA YA HABARI MAELEZO, TAREHE 16 SEPTEMBA 2013


*      Wakurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,
*       Ndugu Waandishi wa Habari,
*      Mabibi na Mabwana.

Ndugu wanahabari,
Napenda kwa heshima na taadhima kutumia fursa hii kwa niaba ya Menejimenti ya TFDA na wafanyakazi wote kwa ujumla kuwakaribisha katika mkutano huu.  TFDA ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyoundwa chini ya sheria namba 1 ya Chakula, Dawa na Vipodozi  Sura 219 kwa lengo la kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi. Hii inamaanisha kuwa wanaolindwa ni sisi sote ikiwa ni pamoja na jamaa zetu na wananchi kwa ujumla.

Ndugu wanahabari,
Leo tumekutana hapa kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu mkakati wa TFDA katika kuwaendeleza wajasiriamali wa chakula kwa lengo lakulinda afya ya walaji, lakini pia kufanya vyakula hivyo kuweza kumudu ushindani wa soko la ndani na nje na kuleta matokeo makubwa sasa.


Ndugu wanahabari,
Suala la usalama wa vyakula ni la msingi kwa sababu lina athari kubwa kiafya, kiuchumi na kijamii.  Hata hivyo, kama hazikudhibitiwa ipasavyo matumizi ya bidhaa hizi yanaweza kuleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kusababisha ulemavu, kupoteza maisha na hata kudhoofisha uchumi wa nchi. Kwa sababu hiyo TFDA kama taasisi iliyopewa dhamana ya usimamizi wa bidhaa hizo inahakikisha kwamba vyakula vinavyouzwa katika soko la Tanzania vinakidhi viwango vya usalama, ubora na ufanisi.
TFDA ina majukumu mengi kwa mujibu wa Sheria. 

Miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na udhibiti wa uhifadhi, usafirishaji, usindikaji, uagizaji na usambazaji vyakula. Katika kutekeleza jukumu lake, TFDA inasajili majengo yote yanayotumika katika usindikaji wa vyakula ikiwa ni pamoja na utoaji wa vibali vya usindikaji, uingizaji na usafirishaji nje vyakula. Majukumu mengine yanayofanywa na TFDA ni pamoja na ufuatiliaji usalama wa vyakula kwenye soko na utoaji wa elimu kwa wadau mbalimbali.

Ufanisi wa utekelezaji wa majukumu haya unawezekana kutokana na  mifumo mizuri ya utendaji kazi iliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kulingana na viwango vya kimataifa vya ISO 9001: 2008.

Ndugu wanahabari,
TFDA kama taasisi ya udhibiti wa vyakula, tunatambua kuwa tuna wajibu wa kuwasaidia wasindikaji wadogo wa vyakula ili waweze kukua na kuzalisha vyakula kwa mujibu wa Kanuni bora za uzalishaji ili viweze kumudu ushindani wa soko la  ndani na  nje kutokana na biashara huria na kuzalisha chakula salama.

Takwimu zinaonesha asilimia 75 ya viwanda vya vyakula nchini ni viwanda vidogo (Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliofanyika 2004/5) ambapo kukua kwa viwanda hivi kutakuwa na mchango mkubwa katika; kuongeza ajira na kipato katika ngazi ya kaya, kukuza kilimo cha mazao ya chakula kutokana na kuwepo na soko la mazao ya vyakula na kuchangia katika pato la taifa.

TFDA inatambua kuwa viwanda vidogo vina nafasi kubwa ya kuchangia katika pato la Taifa kutokana na uwingi wake lakini pia vinaweza kutoa mchango mkubwa katika kuleta athari za kiafya ikiwa bidhaa zake hazitakidhi viwango vya usalama na ubora.

Ndugu wanahabari,
Kwa kuzingatia mambo hayo niliyotaja, TFDA imeamua kuja na mkakati wa kuwafundisha wajasiriamali wadogo wa vyakula ili kuwawezesha wasindikaji hawa kujua sheria, kanuni na miongozo inayohusu usindikaji wa chakula salama pamoja na kuongeza kiwango cha uzingatiaji wa kanuni bora za uzalishaji wa vyakula.
Hadi sasa mafunzo hayo yametolewa kwa wajasiriamali 417 kutoka katika Kanda zote katika mikoa ya Dar es Salaam (90), Singida (44), Mbeya (76), Arusha (54), Dodoma (98) na Mwanza (55).

Ndugu wanahabari,

Aidha, kutoka mwaka 2012/13, TFDA imekuwa inaendesha mpango wa majaribio kwa wasindikaji wadogo wa mafuta ya alizeti mkoani Singida  ili kuelekeza namna ya kuboresha uzingatiaji wa matakwa ya Sheria kuhusu misingi ya usafi na uzalishaji bora.
Mpango huu umehusisha hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na;
i.   Kufanya tathmini ya kiwango cha uzingatiaji wa sheria
ii. Kuainisha maeneo yenye mapungufu
iii.  Kuandaa mafunzo yanayozingatia mapungufu yaliyojionesha
iv.  Kuwasilisha taarifa ya tathmini kwa wadau pamoja na wasimamizi wa sheria katika eneo husika
v.    Kukubaliana namna ya kutatua upungufu na kuwa na ratiba ya utekelezaji kwa mambo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu
vi.  Ufuatiliaji wa makubaliano
vii. Tathmini ya jumla kwa makubaliano ya muda mfupi na wa kati ili kujua kiwango cha utekelezaji.
Lengo la mpango huu ni kusambazwa nchi nzima ikiwa utaleta matokeo mazuri kwa mkoa huu wa Singida ambao ni wa majaribio ifikapo mwaka 2016/17.

Ndugu wanahabari,

Kwa kuhitimisha, TFDA inatoa shukurani kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkiuonesha katika kutoa taarifa za kiudhibiti pale inapotokea pamoja na kuelimisha jamii.

Rai yetu kwenu ni kuendelea kutumia kalamu zenu katika kuwaondolea hofu wananchi kuhusu usalama na ubora wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba vilivyopo katika soko kutokana na mifumo thabiti iliyowekwa na TFDA.

Aidha, tunatoa wito kwa wananchi kwamba ikiwa mtu atabaini au kuwa na mashaka juu ya usalama na ubora wa bidhaa hizo basi asisite kuwasiliana nasi kupitia ofisi zetu za Makao Makuu na za Kanda zilizopo Extenal Mabibo, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma na Ofisi za Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya au kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi kilicho jirani naye.

Asanteni kwa kunisikiliza!
Previous Post Next Post

Popular Items

WAKUU WA USALAMA KUHOJIWA KENYA