Jua Umuhimu wa Tamasha la Filamu Dar "DFF"




Kwa muda mrefu tamasha la filamu la kimataifa la filamu Zanzibar, ZIFF limekuwa likifanyika kwa ufanisi na maandalizi makubwa ya kuvutia. Hatuwezi kubeza umuhimu wa tamasha hilo kwa Tanzania hasa kwa jinsi ambavyo hukutanisha filamu za kimataifa, watu muhimu kwenye kiwanda cha sinema duniani na jinsi tamasha linavyoitangaza Tanzania na kivutio cha watalii.



Lakini licha ya kuwa na mafanikio makubwa na kuhusisha wadhamini wengi, ZIFF si tamasha linaloweza kutoa mchango wa moja kwa moja wa maendeleo ya filamu za nyumbani. Tamasha hilo limekuwa sehemu iliyotawaliwa na uzungu mwingi na kuzifanya filamu za Tanzania kuwa mtoto aliyegeuzwa wa kambo kwenye familia ya wazazi wake mwenyewe.

Huenda ujio wa Dar Filamu Festival, DFF unaweza ukawa mkombozi kwa filamu za Kiswahili za hapa nyumbani. Ndio tamasha linalohitajika zaidi kwanza ili kuzipa nafasi zaidi filamu za nyumbani zishindane zenyewe kabla ya kushindanishwa na zile za kimataifa.

DFF Linaweza kuonekana dogo kwakuwa ndio linaanza, lakini kwa muda mrefu Tanzania ilihitaji jukwaa moja kubwa kama hili la kujivunia filamu zetu (hivyo hivyo zilivyo) na kuwafanya watu wazipende na kuthamini vyao kwao.

Hizi ni sababu kwanini tamasha hilo ni muhimu zaidi kwa Tanzania kuliko ZIFF

1. Ni tamasha la filamu za Tanzania peke yake. Waandaji wa tamasha hilo wamedai pia hapo baadaye kuongeza zaidi wigo na kushirikisha nchi zingine, lakini filamu zitakazohusishwa ni za Kiswahili pekee yake.

2. Linafanyika kwenye kitovu cha filamu Tanzania. Waigizaji, watayarishaji na makampuni yote ya filamu Tanzania yapo Dar es Salaam, tamasha limewekwa kwenye center ya Bongo Movies.

3. Lengo lake ni kuwafanya Watanzania wapende filamu za Tanzania. Tamasha hili litakuwa na kazi ya kuwafanya watu wapende filamu zao za nyumbani na kuzithamini.

4. Limekuja katika katika muda ambao soko la filamu limekua na lina mashabiki wengi. Ni sehemu ambapo mashabiki watawaona kwa ukaribu waigizaji wawapendao.

5. Siku za mbeleni litaongeza soko la filamu za Kiswahili kwa kukutanisha na wadau wengine wa filamu hizo wa Afrika Mashariki.

6. Elimu kuhusu filamu za Kiswahili katika muktadha wa Kitanzania kwakuwa tamasha litaambatana na utoaji wa semina kwa wadau wa filamu kwa asubuhi ambapo madarasa yataendeshwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sanaa kuhusu Uandishi wa Muswada, Uigizaji na Uongozaji wa filamu.

Tamasha hilo lililoandaliwa na kampuni ya Haak Neel Production kwa kushirikiana na mtandao wa habari za filamu wa www.filamucentral.co.tz litafanyika kwenye viwanja vya Posta Kijitonyama, kuanzia tarehe 24- hadi 26, September,2013.



 Credit via: Bongo5 
Previous Post Next Post