Waazimia kuunda timu ambayo itamshawishi January Makamba kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Morogoro. Viongozi wa Vyuo Vikuu 21 nchini wameazimia kwa kauli moja kuunda timu ndogo itakayokwenda kumshawishi Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Mbeya, Theonest Theophil alisema hilo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa siku mbili na kuwashirikisha marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu na maspika wa vyuo 21 nchini.
Theophil alisema mkutano huo uliyapigia kura majina matatu yakiwamo ya wabunge wengine wawili vijana; John Mnyika na Zitto Kabwe na kwamba Makamba alipitishwa kuwa chaguo lao baada ya kupata kura 70 kati ya 105 zilizopigwa. Alisema Zitto alipata kura 20 na Mnyika kura tisa, huku kura tisa zikiharibika.
Alisema viongozi hao wamepanga kutembea nchi nzima na kuwashawishi Watanzania kumuunga mkono Makamba endapo ataafiki kuwania nafasi hiyo ya urais, huku wakidai kwamba wamechoshwa na viongozi wenye visasi na uadui ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi kulumbana na kupambana badala ya kuwatumikia wananchi.
Theophil alisema mkutano huo ulilenga kujadili mustakabali wa nchi katika masuala ya ubora wa elimu na vihatarishi vya amani ambavyo vinatokana na chuki za kidini, siasa na visasi. Pia walijadili tatizo la ajira kwa vijana, ukuaji wa uchumi na mchakato wa Katiba Mpya ambao alisema hivi sasa ni kama umetekwa na ushabiki wa kisiasa.
Theophili alisema walibaini kwamba ili kukabiliana na changamoto zilizopo lazima nchi iwe na uongozi thabiti, hivyo walimchagua Makamba kama mmoja wa viongozi wenye sifa za kushika wadhifa wa urais kwa kuzingatia sifa alizonazo.
Alizitaja baadhi kuwa ni kuonyesha uwezo na ujasiri katika nafasi za uongozi alizowahi kushika na uadilifu, kwani hajawahi kuhusishwa na vitendo vya rushwa na ufisadi katika uongozi wake.
Kwa upande wake, Said Ngolola kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu limekuwa likiathiri mfumo wa elimu ya juu nchini, kutokana na kushindwa kwa waliopewa dhamana ya kusimamia suala hilo hali ambayo imekuwa ikileta migogoro isiyoisha..
Mkutano wa viongozi hao uliandaliwa na kufadhiliwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya FPID inayojihusisha na mapambano dhidi ya maradhi, ujinga na umaskini yenye makao yake makuu Dar es Salaam.
Katibu wa asasi hiyo, Frances Ndunguru alisema asasi hiyo haina uhusiano wowote na wanasiasa, bali lengo ni kuwezesha makundi mbalimbali ya kijamii kukutana na kujadili masuala yenye masilahi kwa nchi.
CHANZO: mwananchi.co.tz
Tags:
Politics