Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewashukia waendesha mashitaka na wapelelezi kesi zinazohusiana na dawa za kulevya kuwa hadi sasa zimefikia 36 lakini hakuna taarifa zake.
Mwakyembe aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye Kipindi cha Jenerali On Monday kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten juzi usiku.
Mwananchi iliwasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka, Elieza Feleshi kuhusiana na hilo, lakini hata hivyo simu yake ilikuwa haipatikani. Hata ilipofika ofisini kwake, ilielezwa kuwa alikuwa kwenye mkutano.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alipotafutwa jana kuzungumzia hali hiyo, simu yake ilikuwa haipatikani.
"Kila anayekamatwa lazima achukuliwe hatua stahiki kwa kosa lake na hakuna sababu ya kuleana wala kuogopana," alisema Dk Mwakyembe ambaye ametangaza kujitoa muhanga kupambana na mtandao wa dawa za kulevya nchini.
Mwakyembe aliyekuwa akizungumzia mapambano hayo aliyoyaanzisha ya dawa za kulevya, alirejea sakata la kuvushwa dawa za kulevya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, JNIA alisema: "Wote tumewafukuza kazi kwa sababu walihusika kupitisha dawa hizo."
Hata hivyo, Mkurungenzi wa JNIA, Moses Malaki akizungumza na gazeti hili, alisema juzi kuwa utaratibu wa kuwapatia barua zao umekamilika na sasa kinachofuata ni utaratibu wa kuunda tume ambao utafanyika wakati wowote kwa ajili ya uchunguzi na kuwahoji.
Wafanyakazi hao wa JNIA, wanatuhumiwa kula njama za kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine.
Dk Mwakyembe alisema pia kuwa watu hao watafukuzwa kazi pamoja na wahusika wengine. "Ule mkanda unaonyesha watu walivyokuwa wakihangaika siku ile pale. Kuna askari anaonekana anasaidia kupitisha mizigo kwenye mashine, huyu askari ni kazi yake hii?
"Wapo watu walikuwa wakihangaika huku na huko, yaani walikuwa hawatulii, ni kama sinema, wengine wako 'bize' na simu badala ya kufanya ukaguzi, sasa tumewafukuza...Najua wapo wengine, nasema kama mtu aliona, alisikia na hakusema naye atakwenda na maji.
Alisema amewasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo. "Nimemwomba Waziri wa Mambo ya Ndani tufanye kazi na lazima tuumalize huu mtandao."
Akizungumzia ukaguzi wa mizigo, Dk Mwakyembe alisema lazima mizigo yote ikaguliwe hata bandarini. "Pale Uwanja wa Ndege kuna mitambo pengine bora zaidi kuliko mahala pengine popote Afrika na kama haitoshi, tuongeze mingine zaidi.Alipoulizwa kama atakuwa na ubavu wa kuzuia 'unga' wa vigogo, Mwakyembe alisema: "Kigogo yeyote atakayejitokeza nitamkamata tu...Ajitokeze sasa hivi aone. Nimeshangazwa na kilo 180 kupita, huu mtandao wa kipuuzi lazima kuuvunja.
"Asije mtu akatarajia kuchekewa, ataondoka. Atakayeruhusu mtu kupita na dawa za kulevya, tukibaini, ataondoka tu. Wako wengi wanatafuta kazi. Tulijiachia vya kutosha, na sasa basi."
Akizungumzia hali ilivyo Bandarini kwa sasa, alisema wameimarisha udhibiti wa upotevu wa makontena. "Hali kwa sasa ni nzuri, ilikuwa aibu, kila siku makontena yanapotea, tulianzisha utaratibu, kontena likipotea kitengo kizima wanakatwa mishahara kulipia," alisema.
Alisema pia kumeanzishwa utaratibu wa kukagua mizigo yote inayoingia na kutoka.
CHANZO: MWANANCHI
Tags:
Social