Watoto wa Msafiri Diouf ndio waliomsaidia baba yao kuacha kubwia ‘Unga’ aliokuwa akitumia toka 1996



Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema tatizo la dawa za kulevya ni Janga la kitaifa, kutokana na ongezeko la watu wanaoendelea kukamatwa wakisafirisha na kuingiza dawa hizo nchini na kuendelea kuwaathiri vijana wengi wanaogeuka kuwa mateja.
Diouf-2
Rapper wa bendi ya African Stars Msafiri Diouf amekiri kuwa miongoni mwa waathirika wa dawa hizo za kulevya toka mwaka 1996. Akiongea na gazeti la MWANANCHI wiki hii Diouf amesema, baada ya kutumia dawa hizo kwa muda mrefu hatimaye alijikuta anakata shauri na kutafuta msaada wa kuacha kutumia baada ya watoto wake wawili kumfanya ajione mkosaji (feel guilty).
Diouf alisema, “Nina watoto wawili, Najma a.k.a Vannesa na Taslim a.k.a Paris’ sasa roho iliniuma sana siku moja watoto wenzao walikuwa wanawaambia baba yenu nyie ni teja. Nilijisikia vibaya kuona watoto wangu watazidi kusakamwa kwa kuambiwa kuwa baba yao (mimi)ni teja.
Hali hiyo ndio iliyonifanya niamue kukata shauri na kwenda Muhimbili nikaonana na Dokta Ayubu ambaye yeye akanipeleka Lutindi, hiyo ilikuwa ni mwaka jana na nilikaa hospitali kwa miezi mitatu lakini toka nimetoka huko nina miezi tisa na bado naendelea kupata ushauri Muhimbili, huwa naenda kila Jumatano na Ijumaa.” Alisema Diouf
diouf-1
Akizungumzia jinsi alivyojikuta ameingia katika utumwa huo wa hiari wa kutumia dawa hizo Diouf alisema
“Nilianza kubwia unga toka mwaka 1996, sikujua kama unga una madhara, awali nilikuwa navuta bangi lakini kuna jamaa mmoja sasa hivi ni marehemu ndio alinifundisha kubwia unga.”
Kuna wakati alikuwa anachanganya unga na bangi. hata hivyo mimi na wenzangu hatukujua kama anachanganya na bangi, kuna siku akatupa bangi bila ya kuchanganya na unga tulivyovuta tukaona mbona ipo tofauti na haileti ulevi sana, tukamuliza hii vipi mbona mbaya akasema sijawachanganyia, tukamuuliza hujatuchanganyia na nini akasema unga, tukamwambia tuchanganyie basi, kweli alipochanganya tukavuta tukajiona kama tuko Ulaya vile, dunia yote ipo mikononi mwako.”
“Kuanzia hapo ndio nikafungua ukurasa mpya wa kutumia dawa za kulenya, nikafikia kipindi nikaacha kuchanganya na bangi, nikawa nabwia na kunusa, wakati ule kete moja ilikuwa ikiuzwa Sh250 sasa hivi inauzwa Sh2,000.”
Hivi karibuni kumeibuka matukio kadhaa ya watanzania kukamatwa wakijaribu kusafirisha dawa za kulevya nje ya nchi na wengine wakijaribu kuingiza nchini. Mwezi huu peke yake (July) watanzania wapatao watano wamekamatwa wakijaribu kusafirisha dawa hizo, tukio la kwanza likiwahusisha wasichana wawili ambao tayari wamefahamika majina yao (kwa mujibu wa NIPASHE) kuwa ni Agnes Gerald (25) pamoja na Melisa Edward (24) waliokamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa OR Tambo nchini Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya zaidi ya shillingi billion 6.


news via: MWANANCHI
Previous Post Next Post

Popular Items