Zaidi ya wananchi 700,000 waishio katika manispaa ya Tanga sasa hawatahitaji tena kupanga foleni ili kulipia ankara za maji. Hii inafuatia ushirikiano baina ya Vodacom Tanzania na mamlaka ya maji safi na maji taka ya Tanga (UWASA) utakaowezesha malipo hayo kufanyika kupitia huduma ya M-Pesa na Airtel Money.
(UWASA) ni mamlaka iliyoundwa kisheria chini ya sheria ya utoaji maji kifungu cha 272 ili kuendesha shughuli za upatikanaji wa maji safi na kusimamia maji taka mjini Tanga.(UWASA) ilianza kufanya kazi zake kama taasisi huru mwezi Januari, 1998.
Huduma ya M-Pesa ina mawakala zaidi ya 40,000 nchi nzima, hivyo kuwezesha urahisi wa malipo ya huduma ya maji kama hii mahala popote pale nchini. Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UWASA,Injinia Joshua Mgenyekwa, alizungumzia jinsi ambavyo kwa kiwango kikubwa wakazi wa Tanga wataepuka usumbufu wa kutumia muda mrefu kwenye foleni za kulipia huduma ya maji na kusema:
"Huduma hizi ni hatua ya kipekee hasa ikizingatiwa kuwa kuanzia sasa muda ambao mteja angeutumia kusubiri kwenye foleni, badala yake atauingiza katika shughuli nyingine za kila siku kama kazi au biashara. Pia kufanya malipo kupitia M-Pesa au Airtel Money kutarahisisha ufanyaji kazi wa mamlaka na kutoa nafasi ya kuongeza ubora wa huduma."
Mkuu wa kitengo cha biashara cha M-pesa Vodacom Tanzania,Bw.Jackson Kiswaga alisema: "Nawahimiza wakazi wa Tanga watumie huduma ya M-Pesa kulipia ankara za maji kutokana na kuwa ni huduma ya haraka na salama. Hii ni njia ya uhakika ya kuokoa muda malighafi muhimu wa muda, na hivyo ni vyema sote kuitumia."
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya maji safi Mkoa wa Tanga,(UWASA) Injinia Joshua Mgenyekwa(katikati)akimshuhudia Mkuu wa kitengo cha biashara cha M-pesa Vodacom Tanzania,Bw.Jackson Kiswaga kushoto akisaini mkataba kwa ajili ya kutoa huduma ya M-pesa kwa wakazi wa mkoa wa Tanga,ambapo watakuwa wakilipia Ankara za maji kwa mara ya kwanza kupitia huduma hiyo na Airtel Money,kulia ni Meneja wa kanda ya kaskazini wa Airtel Bw.Stephen Kimea.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya maji safi(UWASA) Mkoa wa Tanga,Injinia Joshua Mgenyekwa(katikati)akibadilishana nyaraka walizosainiana zinazohusu makubaliano ya kutoa huduma ya M-PESA na Mkuu wa kitengo cha biashara cha M-pesa Vodacom Tanzania,Bw.Jackson Kiswaga.Ambapo wakazi wa mkoa huo watakuwa wakilipia Ankara za maji kwa mara ya kwanza kupitia huduma hiyo na Airtel Money,kulia ni Meneja wa kanda ya kaskazini wa Airtel Bw.Stephen Kimea.
Baadhi ya wafanyakazi wa taasisi ya maji safi Mkoa wa Tanga,(UWASA)wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania na Airtel,mara baada ya kusainiana mkataba wa kampuni hizo mbili kutoa huduma ya malipo ya Ankara za maji kupitia huduma ya M-PESA NA Airtel Money.