BANDARI YA DAR ES SALAAM NI KICHOCHEO CHA UCHUMI – BENKI YA DUNIA





Na VOA



Tanzania na mataifa jirani ya Afrika Mashariki yanatajwa kuwa yanaweza kuboresha pato la ndani la mwaka – GDP – kama yatachukua hatua za kuboresha ubora wa bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ripoti mpya iliyopewa kichwa cha ‘Opening the Gates: How the port of Dar es Salaam can transform Tanzania’ iliyoandikwa na Jacques Morisset, mchumi mkuu wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Uganda na Burundi, Tanzania na majirani zake wanaweza kuongeza pato lao la ndani kwa kiwango kikubwa.
Ripoti hiyo inasema Tanzania inaweza kuongeza pato lake la ndani kwa kiasi cha dola bilioni 1.8 na nchi jirani zinaweza kupandisha pato la ndani kwa dola milioni 830 kwa mwaka, kiwango ambacho kinaelezewa ni hasara iliyotokea mwaka 2012.


Ripoti hiyo inasema kuwa bandari ya Dar es Salaam iko katika njia kuu ya biashara ya Tanzania kwa asilimia 90, na inashughulikia bidhaa zinazogharimu dola bilioni 15 kwa mwaka, sawa na asilimia 60 ya pato la ndani la Tanzania kwa mwaka 2012.


Bandari hiyo pia inaelezewa kuwa inatumiwa na majirani sita wa Tanzania, ambao nchi zao hazina bandari, nchi hizo ni Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.


Mwaka 2012 pekee, ripoti inasema hasara ya jumla inayoelezewa ambayo imetokea katika bandari hiyo imefikia dola bilioni 1.8 kwa uchumi wa Tanzania na dola milioni 830 kwa nchi jirani. Hasara ambayo ni sawa na asilimia saba ya pato la ndani la mwaka la Tanzania, na kwa kiasi kikubwa imeathiri wanunuzi wa ndani, biashara na mashirika ya serikali.


Moja ya sababu ambazo inaelezewa zimechangia katika hasara hii ni utendaji mbaya wa bandari ya Dar es Salaam ambao umezigharimu nchi nyingine jirani nazo kupata hasara, na hivyo kulazimika kulipa fedha zaidi kwa bidhaa zinazoagiwa kutoka nje, ikiwemo bidhaa za msingi kama vile mafuta ghafi, simenti, mbolea na madawa.


Moja ya vigezo vilivyoelezewa katika ripoti ambavyo vinachangia katika kusababisha hasara ni pamoja na uchelewesho unaozikabili meli ambazo zinafika katika bandari ya Dar es Salaam. Katikati ya mwaka 2012, meli zilisubiri kwa takriban siku 10 ili kuweza kuruhusiwa kutia nagan na siku 10 nyingine za ziada ili kuweza kushusha mizigo. 




Rushwa pia imetajwa kuwa ni kigezo kingine kinachochangia katika utendaji mbaya wa Bandar, kama chanzo cha utendaji mbaya na kusababisha hasara kubwa.
Previous Post Next Post