RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) amewataka wadau wa mchezo huo kuwa watulivu kwa vile tofauti zilizojitokeza kati ya Shirikisho na Serikali zitamalizwa kwa taratibu za mpira wa miguu. Amesema nia ya TFF ni kuhakikisha Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) haliifungii Tanzania kwani tayari Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alishaahidi kuwepo kikao kati yake na viongozi wa TFF kitakachofanyika Jumanne
(Machi 19 mwaka huu).“Suluhu itapatikana kwa mazungumzo kati ya Wizara na TFF. Naamini suala hili tutalimaliza baada ya kikao cha Machi 19 ambacho kimepangwa na Waziri kutokana na maombi ya TFF,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa tatizo lilianzia kwenye mchakato wa uchaguzi ambao umesimamishwa na FIFA. FIFA ilisimamisha Mkutano Mkuu wa uchaguzi baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika, na yenyewe kuahidi kutuma ujumbe wa kushughulikia suala hilo.
Rais Tenga amesema lisingetokea tatizo hilo, TFF tayari ilishaitisha Mkutano Mkuu ambao ungefuatiwa na uchaguzi. Lakini kwa vile FIFA ndiyo iliyosimamisha mkutano huo, TFF inalazimika kusubiri hadi FIFA itakaposhughulikia suala hilo na kutoa maelekezo ikiwemo lini mkutano ufanyike.
Amesema kwa kuamini tatizo hilo litamalizwa ndani ndiyo maana TFF hadi sasa haijapeleka FIFA maagizo ya Waziri Dk. Fenella ya kutengua marekebisho ya Katiba ya TFF ya mwaka 2012, kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya Katiba na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi, kwani ingefanya hivyo Tanzania ingefungiwa mara moja.
TFF inasisitiza kuwa FIFA ilijua tatizo la Serikali kutoa maagizo kwake kupitia vyombo vya habari, hivyo kumuandikia Rais Tenga na kueleza msimamo wake iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu.
Uhalali wa kuwepo kwa barua ya FIFA kwenda kwa Rais Tenga juu ya suala hilo ulihojiwa pia na mwandishi wa Reuters, Brian Homewood baada ya kusoma kupitia vyombo vya habari nchini kuwa Shirikisho hilo huenda likaifungia Tanzania ikibainika Serikali inaingilia shughuli za TFF. Mawasiliano kati ya FIFA na mwandishi huyo ambapo majibu yake pia TFF ilipewa nakala yameambatanishwa katika taarifa hii.