TAMKO LA UDASA JUU YA UCHOCHEZI WA UDINI TANZANIA


DSC00032 fed53

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 2/3/2013
Wapendwa waandishi wa habari. Tunaomba kupitia ninyi tuweze kuongea na watanzania wenzetu kuhusu hali ya amani ilivyo nchini mwetu kufuatia kila aina ya dalili ya watanzania kukosa uvumilivu wa kidini. Tunatambua kuwa serikali yetu imefanya mambo mazuri mengi tu nchini, hilo hatuna mashaka nalo; hata hivyo kama watanzania tunadhani kuna baadhi ya mambo hayaendi sawa. Hivyo basi, tunaomba kuchukua nafasi hii kuelezea wasiwasi wetu

kuhusu migogoro hii ya kidini inayozidi kukua nchini.
Migogoro hii ilianza kuvuka kama moshi lakini sasa inaanza kulipuka na kusambaa zaidi.
Tumeshuhudia uchomaji moto wa kanisa kule Mbagala, kumwagiwa tindikali shekhe mmoja
kule Zanzibar na Shekhe mwingine kuuawawa, kuchomwa makanisa Zanzibar, kupigwa
risasi viongozi wa kikristo kule Zanzibar na pia mgogoro wa kuchinja huko Geita ambako
tumeshuhudia mchungaji mmoja akiuawa.
Mbali na hayo, kuna matukio kadhaa kwenye shule zetu za sekondari yakihusisha migogoro
ya kidini kati ya wakristo na waislamu. Haya tumeshahudia yakitokea sekondari za
Bagamoyo, Ndanda, Kibiti, Ilboru na kwingineko. Pia yapo malalamiko yasiyo rasmi kuhusu
udini kwenye sehemu za kazi na kwenye taasisi mbalimbali za serikali. Wapo wanaodai
kuwa baadhi ya taasisi binafsi, za kidini na hata za serikali zinazohudumia watanzania wengi
zimekuwa zikiajiri wafanyakazi kwa misingi ya kupendelea dini fulani fulani. Jambo hili hata
kama ni la kuzungumzwa tu, ni vema likafanyiwa kazi maana hisia hizi zikipanuka hujenga
chuki na kusababisha watanzania wasielewane.
Kwanini haya yanatokea?
Sisi wanajumuiya ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tunaamini, kama taifa,
kuna mahali tumechepuka na kuacha misingi tuliyoachiwa na Baba wa Taifa katika ujenzi wa
taifa imara na lenye umoja. Kuna sababu kadhaa zilizotufikisha hapa tulipo, nazo ni:
1) Wanasiasa na watanzania wengi tunafuata dini zetu kwa hisia zaidi pasipo kufikiri
kwa kina kuhusu yale tunayoyafanya. Tumesahau kabisa kuwa dini ni kwaajili ya
kutuhusianisha na ulimwengu ujao tusioujua. Tunapaswa kumheshimu na kumthamini
kila binadamu aliyeko hapa duniani. Kwa bahati mbaya baadhi yetu tunadhani kuwa
ulimwengu huu umeumbwa kwaajili ya dini fulani na binadamu wengine hawana haki
ya kufurahia maisha yao hapa duniani. Tunataka kutumia dini zetu kumiliki utawala
wa dunia hii.
Dini zetu zimekuwa mtaji kwa baadhi ya wanasiasa na vyama vyao. Inasikitisha kuwa
hakuna jitihada za kutosha zilizofanyika kuzuia wanasiasa kutumia dini kama sera
au ajenda ya katika kupata kura. Baadhi ya wanasiasa wameingia madarakani kwa
kutumia udini na ukabila na hivyo hali inapofikia watanzania kuanza kuchukiana kwa
misingi ya dini wanakosa nguvu na ujasiri wa kukemea na kuzuia haya kwakuwa nao
wamepitia njia hiyo.
2) Sababu ya pili ni kwamba hivi sasa umaskini nchini umekuwa wa kiwango cha juu.
Kila mtu anatafuta jawabu la umaskini wake kwa kudhani kuwa umesababishwa
na mfumo ulio nje ya maisha yake na ya serikali. Katika hali hii wamejitokeza
watanzania wenzetu wanaotafuta majibu mepesi kwa kusingizia kuwa wamekuwa
maskini kwasababu ya dini nyingine. Hali hii imesababishwa na ukosefu wa elimu
kiasi kwamba watanzania wengi wanashindwa kuwa na uwezo wa kuchambua
mambo kimantiki na badala yake wanaamini bila kuchuja lolote wanaloambiwa na
viongozi wa dini au mwanasiasa au mwanaharakati. Ni vema watanzania wakajua
kuwa ajenda ya udini si ya dini fulani bali ni ya makundi machache ndani ya taasisi
zetu za dini. Tusibebeshe lawama za udini kwa dini fulani bali tuelewe kuwa udini
umekuwa ni mtazamo ya watu wachache ndani ya dini zetu.
3) Tatu, watanzania tumeanza kupoteza uelewa kuhusu madui wetu wa asili ambao ni
ujinga, umaskini na maradhi, na tumeongeza adui mwingine ambaye ni imani ya
mwingine. Tumeacha kuelekeza nguvu zetu katika kupambana na maadui hao watatu
na tunaelekeza nguvu zetu kupambana na dini nyingine ambazo kimsingi haziwezi
kuwa sababu ya matatizo yetu ya kila siku.
Kwa bahati mbaya tunashindwa kuelewa kuwa dini hizi kuu mbili za kikristo na
kiislamu ni dini zilizozaliwa sehemu mmoja baadaye zikasambaa sehemu tofauti
na kuchukua utamaduni tofauti. Hatimaye tunachokiona sasa, ndugu wa ukoo na
hata kabila moja waliotokana na historia moja, utamaduni mmoja na lugha moja
wamefanywa maadui kwasababu wanafuata dini tofauti.
4) Jambo la nne, nchi yetu imeruhusu uhuru wa kuanzisha taasisi za dini pasipo kuwa na
usimamizi wa karibu. Taasisi nyingi za kidini zimeibuka nchini na zimekuwa chanzo
kikubwa cha kuwagawa watanzania kwa misingi ya kidini. Umoja wetu unapotea
kwasababu baadhi ya taasisi za kidini zilizopo zinawagawanya watanzania kwa
misingi ya dini. Taasisi nyingi za dini zinafundisha mbinu na namna ya kuwakabili
waumini wa dini nyingine badala ya kuhimiza upendo na mshikamano miongoni mwa
watanzania.
Baadhi ya viongozi wa taasisi hizo wamewafanya watanzania mtaji wao kwa
kuwachochea wafuasi wao kuwachukia wengine kwa lengo la kutimiza haja zao
binafsi. Watanzania tunapaswa kuzinduka na kuchukua tahadhari dhidi ya watu
wanaotuchonganisha. Tukumbuke kuwa kiongozi wa dini anayekuambia kuwa dini
fulani ni ya kishenzi na wafuasi wake ni wa kishenzi basi mtu huyo si mtumishi wa
Mungu bali anatumikia maslahi yake.
Baada ya kueleza sababu zilizotufanya tufikie hapa tulipo sasa, sisi wanataaluma wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam tunapendekeza mambo yafuatayo:
1) Serikali isimamie na kudhibiti vyombo vya habari vya kidini vinavyochochea
chuki za kidini. Inasikitisha kuwa serikali iliyosheheni wataalamu wa kila aina
inashindwa kutambua madhara ya uchochezi wa vyombo vya habari. Watanzania
tunapaswa kujifunza kuwa hata mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda hayakuanza
siku moja, yalichochewa na vyombo vya habari kwa muda mrefu na vyombo hivyo
vilihamasisha pia mauaji hayo.
Hata hapa nchini kwetu, serikali isipokuwa tayari kukemea na kufungia vyombo
vya habari vinavyotumia udini kuleta uchochezi, ipo siku watanzania watauana
sana na nchi itapoteza heshima yake ya kuwa taifa la amani na tutakuwa wakimbizi.
Tunaishangaa serikali inaweza kuyafungia magazeti yanayoikosoa lakini haiko tayari
kuyafungia magazeti yanawachochea watanzania.
Tungependa ujasiri unaotumika na vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata
wanaoandika ujumbe wa vitisho kwa viongozi wa kisiasa nchini utumike pia
kuwakamata wanaochochea uvunjifu wa amani. Kama tunaweza kuwalinda viongozi
dhidi ya vitisho kwa maisha yao binafsi kwanini tushindwe kulilinda taifa letu kwa
kutumia nguvu hizo hizo za kuwatumikia wanasiasa?
2) Pia tunatoa wito kwa wanasiasa na watanzania kwa ujumla kuwakataa wale
wanaotafuta vyeo mahali popote pale, iwe kwenye vyama vya siasa au taasisi,
kwa kutumia udini kama kigezo cha kutaka kuchaguliwa. Ni wakati muafaka sasa
kuhuisha yale yote yatakayoleta mtangamano wa kitaifa. Kama taifa tumeacha
misingi mizuri ya ujenzi wa taifa tuliloachiwa na waasisi wa taifa hili.
3) Jambo jingine ni kuhamasisha na kusimamia sera ya elimu sawa kwa wote. Elimu
yetu ya sasa imejenga matabaka makubwa miongoni mwa watanzania na matokeo
yake matabaka haya yanajitokeza zaidi katika sura ya udini. Kutokana na hali hii
watanzania wengi waliokosa elimu wanadhani kuwa wenzao wa dini nyingine
wanafanikiwa kwasababu ya upendeleo wa kidini. Kwa kusisitiza katika elimu,
itakuwa rahisi kwa watanzania kuelimishwa kuwa chuki za kidini si msingi wa
dini zetu tofauti na ilivyo sasa ambapo ukosefu wa elimu unawafanya wengi kuwa
waathirika wa mafundisho potofu.
4) Pia tunaisihi serikali iwachunguze viongozi wa baadhi ya taasisi za kidini
zinazowahamasiha wafuasi wake kufanya vitendo vya uhalifu. Ni vigumu sana
kuwadhibiti wafuasi wa taasisi ya kidini ambao wameshakuwa na nguvu ya
kuungana na kufanya jambo lolote baya. Tuna wasiwasi kuwa baadhi ya viongozi
wa taasisi hizo wanatumika na watu wa nje kuvuruga amani yetu. Kwa bahati mbaya
viongozi hawa wanajua wazi kuwa amani ikivurugika nchini wao wanazo sehemu za
kukimbilia wakati ndugu zetu wakiendelea kuuana.
Wito wetu kwa watanzania wenzetu ni kwamba wajue kuwa viongozi wa kidini
wanaowachochea kuwachukia wengine hawana nia njema na taifa na maisha yao.
Watatuacha tukiliangamiza taifa huku wao wakiwa salama. Ni vema watanzania
wakajua kuwa sababu ya umaskini na matatizo ya kimaisha hayajasababishwa na
waumini wa dini nyingine bali mfumo wetu mbovu wa utawala unaoacha kukua kwa
matabaka ya kijamii. Tukishirikiana sote kupambana na umaskini hakutakuwa na
sababu ya kuchukiana. Pia, ni muhimu sasa, kila dini iendeshe maswala yake bila
kutaka kubebwa na serikali.
Asanteni sana
Previous Post Next Post