WAKATI aliyekuwa msanii wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba akifikisha mwaka mmoja mwezi ujao tangu alipofariki dunia,msanii mkongwe wa filamu nchini,Sabrina Rupia maarufu kwa jina la (Cathy) ameelezea machungu yake kwenye filamu ya mwisho ya Kanumba.
Akizungumza na Mwandishi wetu Jr BOTEA hivi karibuni Cathy alisema kwamba, kati ya filamu zinazomtoa machozi kila wakati ni filamu ya Power of Love aliyocheza na marehemu Kanumba.
"Power of Love ndiyo filamu ya mwisho ya Kanumba, kila mshiriki katika filamu hiyo alitumia ujuzi wa hali ya juu, "alisema Cathy nakuongeza:mbali na Kanumba pia yumo marehemu Sharo Milionea".
Alisema katika filamu hiyo alishiriki kama shangazi yake Irine Poul ambaye alikuwa mpenzi wa Kanumba, lakini kwakuwa Kanumba alikuwa maskini wa kutupwa basi akawa anamuuza binti yake kwa mwanaume tajiri ili apate pesa.
Katika Filamu hiyo pia Pacha Mwamba alishiriki kama tajiri aliyekuwa anamtaka Irine, na kumfanya binti huyo kuachana na Kanumba aliyekuwa maskini huku marehemu Sharomilionea akishiriki kama rafiki mkubwa wa Kanumba.
"Power Of Love ni filamu pekee ambayo imeniachia kumbukumbu kubwa kuliko filamu zote zilizocheza na Kanumba,ni filamu iliyojaa ustadi mkubwa, chuki na huzuni".
"Power Of Love inazungumzia maisha halisi ya binadamu wanaopenda pesa wanaothamini pesa kuliko utu ama mapenzi, katika fikamu hiyo nakumbuka nilivyokuwa simpendi Kanumba kutoka na umasikini wake wakati akimtaka mtoto wa Kaka yangu"anafafanua Cathy.
Akizungumzia siku ya uzinduzi wa filamu hiyo Cathy anasema kwamba ingawa hajawa na uhakika zaidi kuhusu siku ya uzinduzi wake lakini anadhani inaweza ikwa tarehe 7/4/2013 siku ambayo Kanumba alifariki dunia.
Kanumba alifariki dunia April 7 mwaka jana, baada ya kuuliwa bila kukusudiwa na msanii mwenzake wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) ambaye hivi sasa yuko nje kwa dhamana akisubiri kesi yake katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.