MADAKRI WA KICHINA WATOA HUDUMA VIJIJINI ZANZIBAR


01
Daktari bingwa wa macho kutoka China akimfanyia uchunguzi mtoto Fatuma juma Mzee wa kijiji cha Uzini walipofika kutoa tiba na uchunguzi kwa wagonjwa mbalimbali,huko katika kituo cha Afya Uzini Wilaya ya Kati Unguja.

04
Timu ya Madaktari bingwa kutoka China wakiwa na wenzao wa Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja,huko uzini Wilaya ya Kati Unguja.


WANANCHI wa mbalimbali wa Wilaya ya Kati Unguja, wameelezea kuridhishwa kwao na huduma za uchunguzi wa kiafya na
tiba zinazotolewa na madaktari wa kujitolea kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
 Wakizungumza na gazeti hili jana wakati wataalamu sita wa magonjwa mbalimbali kutoka China wakitoa huduma hizo katika kituo cha afya Uzini, wananchi hao walisema, mpango huo ni mzuri kwani unawapunguzia mzigo wa kufuata huduma mjini na kuchukua muda mrefu wakiwa nje ya vijiji vyao.
 Hamad Juma, mkaazi wa Mgenihaji, alisifu ubora wa huduma zinazotolewa na madaktari hao, na kusema tiba zao ni mjarabu kwnai zimemsaidia sana kupata nafuu matatizo ya macho yanayomkabili.
 “Kwa muda sasa nimekuwa nikitibiwa na madaktari kutoka China katika hospitali kuu ya Mnazimmoja badaa ya kuchomwa jichoni na kitu chenye ncha kali, na leo wamekuja hapa nami nimefuata sawa zaidi”, alifahamisha.
 Naye Mtumwa Jabu Khamis, aliyempeleka mtoto wake mwenye matatizo ya kifua, alisema hatua hiyo ni muhimu na inafaa ifanyike kila kipindi kifupi ili kuwafikia wananchi walio wengi na ambao hawana uwezo wa kufuata huduma hizo mjini.
 Akizungumzia ujio wa madaktari hao, Sheha wa shehiya ya Uzini Vuai Mgeni Vuai, alisema utaratibu unaofanywa na madaktari hao kupitia Wizara ya Afya, unawapa faraja wananchi wa vijijini, kwa kuwaondoshea usumbufu wa maradhi yaliyoficha na hatimaye kupatiwa tiba.
 Alitoa wito kwa wananchi wanapopata taarifa za kufikiwa na madaktari bingwa wa maradhi mbalimbali, wasipuuze kwenda kufanyiwa uchunguzi, kwani huenda wakawa wanaishi na maradhi ambayo hayajajitokeza.
 “Siku hizi kuna maradhi mengi, mengine hatuyajui mpaka tuchunguzwe, hivyo ni vyema kunapokuwa na huduma kama hizi, wananchi wafike ili kuchunguzwa na kuelezea matatizo ya kiafya waliyonayo ili yawahiwe mapema”, alisisitiza Sheha huyo.
 Mapema, kiongozi wa timu ya madaktari hao Dk. Lu Jian Lin, alisema mpango huo unaofadhiliwa na Serikali ya China, unalenga kuwasaidia wananchi wa Zanzibar kuimarisha afya zao ili waweze kushiriki shughuli mbalimbali za kiuchumi.
 Alieleza kuwa, serikali ya nchi yake inatambua uhaba wa madaktari unaozikabili hospitali na vituo vya afya vilivyoko vijijini, hivyo imeamua kwa makusudi kuandaa programu hiyo ya kupeleka huduma katika maeneo hayo Unguja na Pemba.
 Aliwashauri wananchi kuchukua tahadhari ili kujiepusha na maradhi mbalimbali, kwa kula chakula bora, kufanya mazoezi ya mwili na kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao kila baada ya kipindi maalum.
 Zaidi ya wananchi 250 kutoka shehia mbalimbali za Wilaya ya Kati, walipatiwa huduma hizo kwa kupimwa na kutibiwa maradhi ya macho, pua, kifua, masikio magonjwa ya akinamama na ya mifupa.    
Previous Post Next Post