Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Leslie Omari
Moshi!!
Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Leslie Omari, amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikana hatia katika tuhuma zinazoangukia katika makosa ya vitendo vya ufisadi.Mbali na kifungo hicho, Mahakama pia imemwamuru mshtakiwa kuilipa Benki ya Exim Sh330 milioni, ambazo kampuni yake binafsi ya African Consulting Group (ACGL), ilikopa kwa kutumia dhamana ya jengo la
makao makuu ya TCB.
Hukumu hiyo iliyokuwa ikivuta hisia za ndugu, jamaa na marafiki wakiwamo watumishi wa TCB, ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Kobelo, huku mkurugenzi huyo akiwa haamini kilichotokea.
Hata hivyo, Hakimu Kobelo alimwachia huru mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Shaddy Kyambile ambaye wakati makosa hayo yakitendeka mwaka 2003, alikuwa Mkurugenzi wa Fedha wa Bodi ya Kahawa yenye makao yake makuu mjini Moshi.
Hakimu Kobelo alisema anakubaliana na utetezi wa Kyambile kuwa alielekezwa na bosi wake (Omari) kusaini nyaraka za kuidhinisha hati za Jengo la Kahawa, ili zitumike kama dhamana kuikopesha ACGL.
Mkurugenzi huyo mkuu wa zamani, ni miongoni mwa wanahisa wa ACGL, akimiliki asilimia 25 ya hisa.
“Mshtakiwa wa pili alisaini nyaraka kwa maelekezo ya bosi wake (Omari) ambaye alimwambia uamuzi wa kuidhamini ACGL ulishapitishwa na bodi ya wakurugenzi wakati si kweli,”alisema.
Akichambua ushahidi huo, hakimu huyo alisema utetezi wa Kyambile unaungwa mkono na maelezo ya kukiri ambayo Omari aliyaandika akisema yeye ndiye aliyemtaka Kyambile kusaini hati hizo.
Kyambile aliyekuwa akitetewa na wakili mashuhuri wa mjini Moshi, Godwin Sandi kwa sasa ni Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Ngorongoro (NCAA).
Akichambua ushahidi uliomtia hatiani mkurugenzi huyo, Hakimu Kobelo alisema ushahidi umethibitisha kuwa ni mhusika mkuu wa ACGL na alikuwa miongoni mwa watia saini benki.
Alifafanua kuwa mahakama imemtia hatiani mkurugenzi huyo mkuu kwa makosa mawili moja likiwa ni la matumizi mabaya ya ofisi na lingine la kutumia madaraka yake kujipatia manufaa.
“Japokuwa kwenye utetezi wake (Omari), alikana saini zake na mwandiko wake katika nyaraka mbalimbali, lakini teknolojia ya kisasa, imethibitisha kuwa ni saini yake na mwandiko ni wake,” alisema.