Waziri Mkuu wa Tunisia Hamadi Jebali amejiuzulu kufuatia kushindwa kuunda serikali ya mpito ili kutatua mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na kifo cha kiongozi mmoja wa upinzani.
Jebali alikuwa ameahidi kujiuzulu kama mpango wake wa kuunda serikali ya wasomi ungekwama.
Jebali ametangaza kujiuzulu kwake baada ya kukutana na rais Moncef Marzouki, akiitaja hatua hiyo kuwa iliyo bora kwa taifa hilo.
Uchumi wa Tunisia ambao unategemea kwa kiasi kikubwa mauzo ya nje barani Ulaya pamoja na utalii, umeathirika kutokana na machafuko nchini humo na migogoro ya kifedha inayowakumba washirika wake wengi wa kibiashara barani Ulaya.
Tunisia imekuwa katika mgogoro wa kisiasa tangu wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu lilipomwondoa madarakani rais wa zamani Zine El Abidine Ben Ali, na hali imekuwa mbaya zaidi kufuatia kifo cha mwanasiasa wa upinzani Chokri Belaid aliyepigwa risasi nje ya nyumbani kwake mnamo Februari sita.