Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Muasisi wa Chama, Mohammed Matipa alipowasili Ofisi ya CCM, Tawi la Tulieni Kata ya Jamhuri Lindi mjini, Feb. 19, 2013.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mama Salma Kikwete akiimba wimbo wa ‘Wanawake na Maendeleo’, kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Tulieni, Kata ya Jamhuri Lindi mjini.
Wakereketwa wa CCM Mwajabu Abdulrahman (kulia) na Saida Mtopa, wakishangilia wakati Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipokuwa akihutyubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Tulieni, Kata ya Jamhiri, Lindi mjini, Feb 19, 2013.
Wanachama wapya wa CCM wakila kiapo baada ya kukabishiwa kadi zao na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mama Salma Kikwete, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Feb 19, 2013, kwenye Kijiji cha Tulieni Kata ya Jamhuri Lindi mjini.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Kata ya Jamhuri Lindi mjini, wakimsikiliza Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete (hayupo pichani), alipozungumza nao katika kikao cha ndani, kwenye Ofisi ya CCM, tawi la Tulieni katika Kata hiyo.
Bi, Fatuma Jaluo (78) akifuatilia kwa makini msafara wa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ulipopita karibu na nyumbani kwake, katika kijiji cha Tulieni, Kata ya Jamhuri wilaya ya Lindi mjini, Feb 19, 2013.
Kina Mama wa CCM, wakishiriki kula kiapo cha mwanachama wa CCM wakati wanachama wapya waliokabishiwa kadi na Mama Salma Kikwete walipokuwa wakipa, kwenye mkutano uliofanyika kijiji cha Tulieni, kata ya Jamhuri wilaya ya Lindi mjini, Feb 19, 2013. Kutoka Kushoto ni Fatuma Mohamed, Aswila Ditopile na Zitta Maliyaga ambaye ni Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Lindi.
Vijana 36 waliokuwa wanachama wa CUF na kuamua kuhamia CCM, wakimsiliza mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipohutubia mkutano wa hadhara jana, Feb 19, 2013, kwenye Kijiji cha Mitandi, Kata ya Mbanja, Lindi mjini.
Baadhi ya waandishi wa habari, waliopo kwenye ziara ya Mama Salma Kikwete mkoani Lindi, wakiwa wameketi kwenye mkeka wakati wa mkutano uliofanyika kijiji cha Tulieni, Kata ya Jamhuri Lindi mjini Feb 19, 2013. Kushoto ni Mwenyeji wa kijiji hicho, Khalfan Dimoso. (Picha zote na Bashir Nkoromo, wa Daily Nkoromo Blog).
Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi
Wanafunzi wametakiwa kuachana na tabia zisizoendana na maadili ya kiuanafunzi ikiwemo utoro na mashindano ya mavazi bali wasome kwa bidii na kutengeneza mazingira ya kujisomea ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao kwani elimu inaweza kuwatoa katika hali duni ya maisha na kuwaweka katika hali nzuri.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipokuwa akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata za Jamhuri, Makonde na Ndoro zilizopo katika wilaya ya Lindi mjini wakati wa ziara yake ya kuwashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumchagua kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM kutoka wilaya hiyo.
Mama Kikwete ambaye pia ni MNEC alisema kuwa licha ya kuwa na tatizo la upungufu wa walimu na vifaa vya kufundishia lakini wanafunzi wengi wa siku hizi ni watoro, hawapendi kusoma, hawawatii wazazi na walimu wao, siyo wasikivu wawapo darasani jambo linalosababisha kutofanya vizuri katika mitihani yao.
“Wanafunzi lazima mtambue kuwa elimu haina mwisho na elimu ndiyo msingi wa maendeleo, someni acheni tabia ya utoro na mkimaliza darasa la saba jiungeni na elimu ya sekondari, baada ya hapo msome hadi chuo kikuu hali hii itasaidia kupata wataalamu wengi zaidi na hivyo kupunguza tatizo la watumishi”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa wazazi aliwataka kusimamia maendeleo ya elimu ya watoto wao na kuhakikisha kuwa wanakwenda shule na kuhudhuria madarasani na kutowaachia jukumu hilo walimu peke yao kwani kama watoto wao hawatasoma ni vigumu kwa mkoa huo kusonga mbele kimaendeleo kwa kuwa maendeleo hayapatikani bila ya kuwa na elimu.
“Maendeleo ya elimu katika mkoa wa Lindi ni mabaya ukilinganisha na mikoa mingine tatizo hili likiachwa kwa muda wa miaka 10 hali itakuwa mbaya zaidi. Suala la ufaulu mdogo wa wanafunzi lisiwakatishe tamaa na kuwarudisha nyuma bali nyote kwa pamoja wanafunzi, walimu, wazazi na viongozi wa Vyama vya siasa na Serikali mchukue hatua za makusudi ili muweze kuinusuru hali hii”, alisema Mama Kikwete.
Tatizo la utoro lilijidhihirisha pale ambapo zaidi ya wananafunzi 33 kutoka shule ya msingi Tulieni na juzi wanafunzi zaidi ya 40 wa shule ya msingi Kikwetu walihudhuria katika mikutano ya hadhara muda wa masomo wakiwa pamoja na wazazi au ndugu zao na Mama Kikwete alipowauliza kwanini hawakwenda shule hawakutoa sababu za msingi.
Aidha Mama Kikwete pia aliwasihi wananchi hao kulima mashamba yao, kupanda , kupalilia na kuvuna kwa ushirikiano kama walivyokuwa wakifanya miaka ya nyuma na kuachana na tabia ya kila mtu kulima shamba lake peke yake kwani kwa kulima kwa ushirika kwa muda mfupi wanalima hekari nyingi tofauti na kulima mtu mmoja mmoja.
Pia aliwataka viongozi wa vyama vya Siasa na Serikali kuacha tabia ya kuchanganya lugha ya Kiswahili na kiingereza wakati wanajibu maswali au kuongea na wananchi kwa kuwa wananchi wengi hawafahamu lugha hiyo zaidi ya lugha ya Kiswahili na hivyo kuwafanya wasielewe mambo mbalimbali ya maendeleo yao.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Jamuhuri Nelson Bebo alisema kuwa wakazi wa kata hiyo wamenufaika na miradi ya kopa ng’ombe lipa ng’ombe, ufugaji wa kuku wa kienyeji na mayai na ufugaji wa mbuzi na kujipatia kipato cha ziada ambacho kimeongeza pato la familia.
Akiwa katika kata za Jamhuri, Makonde na Ndoro Mjumbe huyo wa NEC alikabidhi kadi kwa wanachama wapya wa CCM 47, Umoja wa vijana 32, Umoja wa Wanawake 52 na Jumuia ya Wazazi 39.