WAZIRI KAGASHEKI NA WAZIRI WA MAREKANI HAYES KUZINDUA KITUO CHA WAGENI - MANYARA


 
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki(Pichani)  na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Marekani Bwana David Hayes kwa pamoja watazindua Kituo cha Wageni cha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (Wildlife Management Area - WMA) cha Burunge Mkoani Manyara na kukikabidhi kwa wananchi. Uzinduzi huo
ambao utafanyika tarehe 5 Februari 2013 ni sehemu ya maadhimisho ya jumuiya za WMA ambazo zilianzishwa nchini mwaka 1998 kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori. 
Pia, ni kuonyesha mafanikio ya Programu ya kuendeleza WMA ambayo inafadhiliwa na Serikali ya Marekani. Vilevile ni ishara kuwa Serikali ya Marekeni itaendelea kuunga mkono shughuli za uhifadhi nchini Tanzania, hususan mapambano dhidi ya ujangili.

Kituo cha Wageni cha Burunge ni sehemu tu ya misaada inayotolewa na Serikali ya Marekani katika Programu ya Kuendeleza WMA nchini kote. Kwa WMA ya Burunge misaada mingine ni ujenzi wa barabara za kufanikisha uhifadhi, kujenga kituo cha askari wa Wanyamapori na kujenga lango kuu la kuingilia kwenye eneo la WMA hiyo.

Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori ni maeneo ya wanyamapori yanayohifadhiwa na kulindwa na Wananchi kwa manufaa yao na taifa. Tangu zianzishwe mwaka 1998 kuna jumla ya WMA 17 nchini ambazo zimesajiliwa rasmi na wahusika kuruhusiwa kufanya matumizi endelevu katika maeneo hayo. Aidha, kuna maeneo 21 ambayo yako katika hatua mbalimbali za kuanzishwa WMA.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
4 Februari 2013

Previous Post Next Post