WAMA YAKABIDHI VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA MILIONI 700



IMG_6982

Na: Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Lindi
Taaasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imeikabidhi hospitali ya mkoa wa Lindi Sokoine  kontena lenye  urefu wa futi 40 lenye mitambo na vifaa vya huduma ya afya vya kisasa  ilivyochangiwa na Shirika linayoshughulika na utoaji wa huduma za kibinadamu la  Project C.U.R.E la nchini Marekani vyenye thamani  ya shilingi milioni mia saba Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika viwanja vya...
Hospitali hiyo ambapo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia  Mwenyekiti wa Taasisi hiyo aliwataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kuvitunza na kuvitumia vifaa hivyo kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi na si vinginevyo.
Akiongea na wananchi wa mkoa huo pamoja na wahudumu wa afya waliohudhuria hafla hiyo  Mama Kikwete alisema kuwa moja ya sababu za vifo vya kina mama wajawazito na watoto ni ukosefu wa huduma bora ya afya.
Alisema kuwa kutokana na tafiti mbalimbali imeonyesha  kwamba kuna maeneo matatu ya ucheleweshaji ambayo huchangia vifo vingi vya akina mama vinavyotokana na uzazi, ucheleweshaji wa kutoa maamuzi majumbani, umbali kutoka vituo vya afya na ucheleweshaji wa kutoa huduma katika vituo vya afya.
“Eneo linalowahusu wahudumu wa afya ni ucheleweshaji wa kutoa huduma ya afya, katika Hospitali hii bado kuna vifo vingi vinavyotokana na tatizo hili nawaombeni mtathmini  tatizo hili na  muweke mikakati ya kuharakisha utoaji wa huduma kwa kuwa hivi sasa vifaa vingi mnavyohitaji vipo”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliendelea kusema kuwa upatikanaji wa huduma bora sio wajibu wa Serikali pekee bali ni wa kila mmoja  kwa nafasi aliyonayo . Kama kila mtu  atatoa mchango wake kikamilifu kwa malengo mengine ya maendeleo ya nchi hakuna mwanamke atakayefariki kwa kukosa huduma ya afya.
Akisoma taarifa ya Hospitali hiyo Kaimu Mganga Mfawidhi Dk. Nicholaus Mmuni alishukuru kwa mitambo na vifaa tiba walivyopewa ambavyo vitasaidia kutoa huduma bora zaidi na kuokoa maisha ya  wananchi kwani walikuwa wanakabiliwa na upungufu wa vifaa hasa vya uchunguzi na vile vya kusaidia kumuhudumia mgonjwa wakati anaendelea kupata huduma ya ndani.
Previous Post Next Post