TUHUMA ZA FEDHA HARAMU ZINAZO MKABILI KAJALA MASANJA NA MUMEWE FARAJA CHAMBO WANA KESI YA KUJIBU


 
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewakuta na kesi ya kujibu Msanii wa Filamu nchini Kajala Masanja na mumewe Faraja Chambo.

Uamuzi huo ulisomwa jana na Hakimu anayesikiliza kesi inayowakabili katika mahakama hiyo, Sundi Fimbo baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka na kuridhika nao na kuona kuwa washitakiwa wanatakiwa kujitetea.

Mahakama hiyo imepanga Februari 8, mwaka huu washtakiwa kuanza kujitetea kulingana na mashtaka matatu yanayowakabili yakiwamo ya kuhamisha umiliki wa nyumba isivyo halali na kutakatisha fedha. 

Aidha upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake baada ya afisa mauzo na masoko wa benki ya Africa nchini (BOA) kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.

Machi 15, mwaka jana Kajala na mumewe walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na kosa la utakatishaji fedha haramu ambapo kwa mujibu wa sheria kosa hilo halina dhamana.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa matatu, kosa la kwanza ni la kula njama ambapo washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa kwa kuhamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam.

Shtaka la pili ni ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010 waliamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007. Shitaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda Aprili 14 mwaka 2010 huku wakijua ni kinyume cha sheria.


Previous Post Next Post