MBUNGE WA JIMBO LA SINGIDA MJINI MOHAMED DEWJI ATOA MSAADA WA BAISKELI KWA WALEMAVU


Mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji akizungumza na mmoja kati ya walemavu watano aliowakabidhi baiskeli za magurudumu matatu kwa ajili ya kuwasaidia kumudu maisha yao hivi karibuni.Pamoja na msaada wa baiskeli hizo, Dewji pia alitoa msaada wa Wheel Chair 24 kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida.Thamani ya msaada huo ni zaidi ya shilingi milioni 14.(Picha na Nathaniel Limu).

Na Nathaniel Limu

Mbunge wa jimbo la Singida mjini, Mohammed Gullam Dewji ametoa msaada wa viti 24 maalum vya wagonjwa (wheel chairs) vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 24 milioni, kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida.

Pamoja na viti hivyo mbunge huyo ametoa msaada wa baiskeli za magurudumu matatu kwa walemavu watano wa jimboni kwake.

Akizungumza kwenye makabidhiano ya msaada huo, Dewji amesema msaada huo ni mwendelezo wa misaada mbalimbali anayoitoa jimboni kwake, kwa ajili ya kusaidiana na serikali kuboresha huduma mbalimbali zikiwemo za sekta ya afya.

Alisema ana aimani kwamba viti hivyo vitasaidia wagonjwa katika hospitali hiyo hasa wale watakaokuwa hawawezi kutembea.

“Tunaochoomba tu ni kwamba viti hivi vitunzwe vizuri ili viweze kutumika kwa muda mrefu”,alisema mbunge huyo.

Awali mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa, Dk.Suleiman Muttani amepongeza mbunge Dewji kwa msaada huo ambao amedai umekuja kwa wakati muafaka.

Dk.Muttani amesema hospitali hiyo inayoendelea kujengwa ina mahitaji mengi na makubwa yakiwemo ya vitendea kazi ambavyo serikali ikiachiwa ifanye peke yake, itachukua muda mrefu kukidhi mahitaji ya hospitali hiyo ambayo itategemewa pia na mikoa jirani.

“Kwa kweli nakushukuru sana mbunge wetu kwa msaada huu wa viti.Tunakuomba usichoke kuisaidia vifaa hii hospitali ya rufaa.Tusaidie pia kuwahamasisha marafiki zako au taasisi mbalimbali ziweze/waweze kutusaidia vitendea kazi kwa kadri ya uwezo wao”,amesema Dk.Muttani.

Kwa mujibu wa Dk.Muttani, hospitali hiyo ya rufaa itakapokamilika itakuwa na majengo 47 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 150 bilioni.

Serikali kila mwaka imekuwa ikitenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi.Kwa utaratibu huo wa kutenga kiasi hicho cha fedha hospitali hiyo itachukua zaidi ya miaka 45 kukamilika kujengwa.

Previous Post Next Post