KWELI NJAA NI HATARI..! YAWAPELEKA WANACHI ZAMBIA KWENDA KUFUATA UNGA


Wananchi wakigawiwa mahindi ya msaada uliotolewa na serikali  katika moja ya mikoa iliyokubwa na uhaba wa chakula,kutokana na ukame katika zaidi ya wilaya 54.Picha na Maktaba 
BAADHI ya wakazi wilayani Nkasi mkoani Rukwa na maeneo mengine ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, wamekuwa wakienda nchini Zambia kununua chakula kutokana na tatizo la njaa lililojitokeza katika maeneo hayo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini upatikanaji wa chakula katika eneo hilo umekuwa mgumu kiasi cha kuchangia kupanda kwa bei ya mahindi kufikia Sh180,000 kwa gunia moja.
Mmoja wa madiwani, Privatus Yoramu alisema kuwa hali ya chakula kwenye eneo hilo ni mbaya na iwapo ikiendelea kwa muda wa miezi miwili kama ilivyo hivi sasa upo uwezekano wa familia nyingi kuanza kulala na njaa.

Yoramu alisema imefikia hatua wananchi hao kwenda kununua unga wa mahindi katika nchi jirani ya Zambia ambako wanafika kirahisi kupitia Ziwa Tanganyika ambako nako hivi sasa baada ya Serikali ya nchi hiyo kubaini chakula kinapelekwa Tanzania imeamua kupiga marufuku.
“Hapa kwetu tunanunua debe moja la mahindi kwa Sh30,000 na unga wa sembe unauzwa kwa kati ya Sh30,000 hadi 35,000 kwa mfuko wa kilo 25,” alisema Yoramu na kubainisha kuwa hata hivyo umekuwa adimu.

Alisema tayari wamepeleka taarifa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmshauri na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi kuwaarifu juu ya uhaba huo wa chakula lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa kupeleka chakula kwenye eneo hilo.
Yoramu ameiomba Serikali iwapelekee chakula cha bei nafuu ili kukabiliana na hali hiyo.
Hali ya upungufu wa chakula pia umelikumba eneo la Kata ya Kipeta kwenye ukanda wa Bonde la Ziwa Rukwa, ambako wananchi wa kijiji hicho waliiomba Serikali kupitia kwa Naibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Aggrey Mwanri kuwapatia chakula cha Msaada baada ya kukumbwa na njaa.
Kata hiyo inakadiriwa kuwa na wakazi zaidi kaya 600 ambapo hali hiyo imejitokeza kutokana na kukosekana kwa mvua za kutosha msimu wa kilimo uliopita.
Kwa mujibu wa mkazi mmoja wa kijiji hicho, Antony Seleman (65) gunia moja la mahindi linauzwa kati ya Sh170,000 na 200,000 huku kilo moja ya unga ikiuzwa Sh17,000 na 20,000 kitu ambacho wao hawezi kumudu kununua.

Hata hivyo, Mwanri aliagiza uongozi wa Serikali mkoani Rukwa kufanya tathmini ili kujua ni idadi gani ya watu wenye mahitaji ya chakula katika kata hivo kabla Serikali haijapeleka chakula cha msaada.
Ilielezwa kwamba sababu nyingine ya kutokea kwa upungufu huo wa chakula licha mvua kuwa kidogo ni pamoja na wafanyabiashara kutoka nje ya mkoa kununua chakula kingi kutoka mkoa wa Rukwa kwa bei ya juu hivyo wananchi wamejikuta wakiuza chakula chote kwa tamaa ya fedha huku uzalishaji ulikuwa kidogo tofauti na takwimu zinazotolewa na maofisa kilimo ambao mara nyingi wanadai mkoa unaziada ya zaidi 400,000.
Shinyanga
Wilaya za Mkoa wa Shinyanga, zinakabiliwa na balaa la njaa kutokana na mvua kuwa kidogo hali ambayo imesababisha kuwa omba omba kwa Serikali ili wananchi wapatiwe chakula.
Wilaya hizo ni Shinyanga, Manispaa, Kishapu na Kahama ambazo kwa sasa wananchi wake wapo katika hali mbaya kutokana na kupata chakula kidogo kwa kile kilichsababishwa na mvua kuwa chache.
Katika wilaya ya mkoa wa Shinyanga inayoongoza kwa njaa ni Wilaya ya Kishapu ambayo kwa sasa wananchi wengi wanakula mlo mmoja kutokana na kutokuwa na chakula cha kutosha.
Akizungumza na mwandishi, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Justin Sheka alisema Halmashauri hiyo imekuwa ikikabiliwa na njaa miaka hii ya karibuni kutokana na kukauka kwa ziwa Kitangili lililoko katika maeneo ya mpakani mwa kishapu na Meatu kwa sababu ya uharibifu wa mazingira ya wananchi wenyewe kulima katika ziwa hilo.

“Hapa mwandishi kinachosababisha njaa katika wilaya yetu inachangiwa na uharibifu wa mazingira hapa, tulikuwa na Ziwa Kitangili ambalo lilikuwa likijaa maji na kusababisha mvua kunyesha lakini kwa sasa limekauka na limesogea huko Singida kutokana na wananchi kulima katika sehemu hiyo,” alisema Sheka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Willison Khambaku alikiri kuwa ni kweli sehemu nyingi za wilaya zina njaa kubwa hali ambayo imesababisha kuagiza Serikali isaidie chakula kwa ajili ya kuwagawia wananchi wanaokabiliwa na njaa, lakini amewaagiza wananchi kulima heka mbili za mtama kila kaya zao ambalo linastahimili ukame.
“Kwa sasa ndiyo mazao yameanza kupendeza kutokana na kamvua kalikonyesha hivi karibuni lakini wilaya yangu bado inakabiliwa na njaa, hivyo hivi karibuni nimewatembelea wananchi na kuwahimiza kulima zao linalostahimili ukame kila kaya heka mbili ili kuondokana na njaa na nimewataka watunze mazao wanayoyapata.
Wilaya ya pili ni Shinyanga ambayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga, Kiyungi Mohamed alikiri kweli ina njaa ambayo inasababishwa na mvua kuwa chache hivyo amehimiza wananchi kulima zao la mtama ambalo ni zao la chakula pamoja na zao la biashara la alizeti ambalo litasaidia kupunguza njaa.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya akizungumzia njaa alisema wilaya yake ina kata 55 kata 28 zina uhaba wa chakula ambazo ni za tarafa ya msalala na kueleza sababu ya ukame huo ni haikuwapo mvua ya kutosha mwaka jana na sababu nyingine ni wananchi kupenda kulima mahindi badala ya kulima mtama na uwele.
Alisema katika maeneo hayo yanazalisha mpunga kwa wingi lakini mvua ilikuwa ni kidogo ndiyo maana mpunga haukuiva vizuri, pia watu hutumia chakula bila kuweka akiba hali hiyo inasababisha njaa, hata hivyo katika wakati wa sasa uhaba upo lakini baadhi ya maeneo wameanza kivisha maharage, viazi hivyo hali si mbaya sana.

Previous Post Next Post