DAWA bandia zinazodaiwa kutibu ugonjwa wa kifua kikuu (TB), zinahofiwa kuingia nchini, ambapo zinadaiwa kutumika kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili tangu mwaka 2011.
Dawa hizo zinazodaiwa kusambaa katika miji mikubwa ya Afrika, zinadaiwa kuanza kuleta madhara kwa watumiaji kwani hazina uwezo wa kuua wadudu wanaosababisha ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wakaguzi kutoka Marekani,dawa hizo aina ya Rifampicin, Antibiotics simesambaa katika miji 19 na 7 nchi zilinunua dawa hizo.
Aidha utafiti huo unaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa TB ambapo asilimia 6.6 ya Afrika, asilimia 10.1 India na 3.9 asilimia katika Brazil, China, Thailand, Uturuki na Urusi watu milioni tisa duniani kote huugua TB.
Miji iliyotajwa kununua dawa hizo bandia ni pamoja na Luanda(Angola),Sao Paulo(Brazil), Beijing(China), Lubumbashi(DRC)na Cairo(Misri). Miji mingine ni Addis Ababa(Ethiopia), Accra (Ghana), Dar es Salaam(Tanzania), Delhi na Kalkata(India),Nairobi(Kenya),Lagos(Nigeria),Moscow(Urusi),Kigali(Rwanda),Bangkok( Thailand) ,Istanbul(Uturuki),Kampala(Uganda) na Lusaka(Zambia).
Utafiti huo unaeleza pia kwamba,dawa hizo zinashindwa kufanya kazi kwa asilimia 16.6 asilimia kwa upande wa Afrika, asilimia 10.1 katika India na 3.9 asilimia katika Brazil, China, Thailand, Uturuki na Urusi.
Kauli ya TFDA
Akizungumza na gazeti hili ili kuthibitisha taarifa hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA), Hiit Sillo alisema kwa sasa hana taarifa yoyote kuhusiana na kuingia kwa dawa hizo bandia nchini.
Mkurugenzi huyo alilitaka gazeti hili kumtafuta Ofisa Uhusinao wa TFDA kwa taarifa zaidi,kwani yeye hayupo kazini kwa kipindi cha wiki moja kwa hiyo asingeweza kutoa ufafanuzi wa suala hilo.
“Siwezi kuzungumza chochote kwani sina taarifa hizo,ila mnaweza kumtafuta Ofisa Uhusiano kwa majibu zaidi mimi nipo nyumbani kwa wiki moja sasa naumwa. Pia sina taarifa juu ya suala hilo,”alisema Sillo.
Gazeti hili lilimtafuta Ofisa Uhusiano wa TFDA,Gaudensia Simwanza ambapo alisema taarifa hizo hazina ukweli,kwani kila wakati wanafanya utafiti ili kutambua dawa bandia na hakuna dawa za kifua kiuu ambazo zimejulikana kama ni bandia kama inavyodaiwa.
Alisema kwa kawaida dawa za kifua kikuu haziuzwi na badala yake zinatolewa bure sasa kupatikana kwa dawa bandia ni kitu ambacho hakiwezekani kwani zinatolewa kwa umakini mkubwa.
“Kwanza ni vyema ikafahamika kwamba dawa za kifua kikuu haziuzwi kwani zinatolewa bure na hazitakiwi kuuzwa, sasa tunashangaa kusikia dawa hizo zimesambaa nchini kwa kipindi cha miaka mwili,”alisema Simwanza.
Alisema TFDA ina utaratibu wa kufanya utafiti wa dawa mbalimbali ikiwa pamoja na dawa za kifua kikuu ambapo kwa kipindi cha mwaka 2011/12 dawa zote za kifua kikuu zilifanyiwa ukaguzi na hakuna dawa iliyotambulika kuwa ni bandia.
“Tunautaratibu wa kufanya ukaguzi wa dawa mbalimbali,ambapo mwaka jana na mwaka juzi tulifanya ukaguzi wa dawa zote za kifua kikuu na hakuna dawa ambazo zilikutwa ni bandia kama inavyodaiwa. Sasa taarifa kama hizo sio za kweli na Watanzania wasiwe na wasiwasi,”alisema.