Balozi Dianna Melrose akifanya mahojiano na mwanahabari Fredy Macha,na Urban Pulse
Picha na Urban Pulse
Na: Freddy Macha
Balozi mpya wa Uingereza nchini Tanzania, Mheshimiwa Dianna Melrose ameeleza furaha yake kuteuliwa kufanya kazi nchini kwetu na kukiri kwamba anauchangamkia wadhifa huo atakaouanza karibuni.Balozi Melrose alikuwa akiongea katika sherehe ya chakula cha jioni iliyofanywa kwa heshima yake nyumbani kwa Balozi wetu wa Uingereza mheshimiwa Peter Kallaghe na mkewe Joyce Kallaghe jijini London Alhamisi iliyopita “Nimebahatika sana.” Alikiri Mama Melrose. “ Watanzania ambao nimekutana nao wana
hulka ya kirafiki na uungwana sana. Ni watu wenye tabia njema na ninahisi nitafurahia sana maisha yangu kwenu. Nitafurahia kwa sababu wenzangu walioshaishi Tanzania muda mrefu wamebakia na mapenzi makubwa ambayo sijayaona kwa Waingereza walioishi nchi nyingine. Wamebakia na kumbukumbu nzuri na mahusiano ya muda mrefu na Tanzania.”
Balozi aliendelea kufafanua kwamba Tanzania inasonga mbele na ni taifa muhimu kwa Uingereza ambaye ni mwekezaji wake mkuu.
“Wakati Balozi Diane Corner aliyenitangulia, alipokutana na Rais Kikwete , Rais alihimiza kwamba mahusiano ya serikali zetu mbili yamefikia mapatano ya juu sana. Hivyo jukumu langu litakua kuimarisha muungano huu.”
Balozi Diane Corner aliyeshika kiti hicho toka 2009 hadi 2013 amehamishiwa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo.
Hafla hii ndogo pia ilihudhuriwa na Afisa Ubalozi wa daraja la pili, Allen Kuzilwa( anayehusika na mahusiano ya kimataifa ya ufadhili wa kimaendeleo na elimu ).
Balozi Melrose mwenye uzoefu mkubwa katika shughuli za ujenzi jamii na mahusiano ya kimataifa alikuwa balozi wa Uingereza nchini Cuba toka 2008 hadi 2012.
Mwanadiplomasia huyu ambaye ni mtaalamu wa lugha za Kifaransa na Kispanyola keshaanza kujifunza Kiswahili na alijaribu kuthibitisha maneno machache aliyoshayanyasua.
Akiwa kijana alifanya kazi shirika linalopambana na umaskini na kupigania haki duniani, Oxfam, mwaka 1980. Oxfam linalohudumia nchi 90 duniani lilianzishwa Uingereza mwaka 1942 mjini Oxford.Melrose alizaliwa Zimbabwe mwaka 1952 akamaliza masomo ya shahada ya kwanza ya lugha- kwa alama za juu (Honours) chuo kikuu cha Kings College, London. Akimkaribisha, Mheshimiwa Balozi Kallaghe alikumbusha kwamba kwenda Tanzania itakuwa changamoto kubwa maana taifa letu linapitia mabadiliko makubwa hasa kutoka kwa vijana, majadiliano ya katiba mpya na hali ya Afrika yenye matukio muhimu sasa hivi.
Mabalozi wengine waliohudhuria ni waheshimiwa Ernest Rwamucyo (Rwanda), Nkwelle Ekaney (Cameroon), na balozi wa zamani Canada (aliyeshastaafu), Antony Carey na mkewe Claire. Vile vile mwakilishi wa Tanzania Standard Chartered Bank, Uingereza, Rweyunga Kazaura, wanachama wa Jumuiya ya Watanzania na Waingereza (BTS) Ron Fennel , mkewe Liz, mhariri wa jarida la Tanzanian Affairs, David Brewin na mfanya biashara wa Kitanzania London (Swift Freight) Bwana Abubakar Faraji.