MTANDAO wa wanawake mkoani Kilimanjaro, umetaka Katiba Mpya iweke usawa katika nafasi tatu za juu za uongozi; Rais, makamu wake na Waziri mkuu ili mojawapo apewe mwanamke.
Licha ya nafasi moja kwa mwanamke, mtandao huo umependekeza katiba iwe katika misingi ya haki, utu, usawa na heshima na kupinga mila na desturi zinazomkandamiza na kumnyima haki mwanamke.
Akizungumza kwenye kongamano la mtandao huo unaoundwa na Azaki 35 kutoka wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro, lililokuwa likitoa maoni ya Katiba Mpya, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Elizabeth Minde alisema ni vyema katiba ikaweka wazi nafasi za uongozi ili mwanamke naye aweze kupewa nafasi ya juu kwenye uamuzi wa nchi.
Minde alisema hivi sasa katiba iko kimya kwenye masuala ya wanawake, ikiwamo haki ya kumiliki mali, kupata elimu sawa jambo ambalo linamfanya mwanamke kukosa thamani kwenye jamii.
Alisema Tanzania imeridhia mikataba na matamko mbalimbali yanayokataza ubaguzi wa aina yoyote, alitolea mfano Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 na Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inatoa haki kwa mwanamke kumiliki, lakini sheria ya mirathi inanyang’anya haki hizo.
Pia, mtandao huo unataka katiba iainishe ushiriki wa wanaume katika afya ya uzazi, ikiwamo kukataza watendaji wabovu kuhamishiwa maeneo ya kazi pindi wanapokosea, badala yake washtakiwe.
Akitoa mada kwenye mkutano huo, Agnatha Rutazaa alisema sekta ya ajira kuna upendeleo mkubwa, kwani kipaumbele kinatolewa kwa wanaume zaidi hata kama mwanamke ana sifa sawa na mwanaume.
Alisema katiba inazungumzia jinsia, lakini kwenye uhalisia hakuna usawa na kutaka Katiba Mpya iweke usawa kati ya mwanamke na mwanaume.