SERIKALI YAELEMEWA NA MIKOPO YA ELIMU YA JUU


SERIKALI imekiri kuelemewa na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa kwa wanafunzi kutokana na ongezeko la wanafunzi wa kidato cha sita na wengine wenye sifa linganifu kupata mikopo hiyo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema hayo bungeni mjini Dodoma jana, wakati akiwasilisha taarifa ya Serikali baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka kupitishwa kwa muswada kuanzishwa kwa mfuko wa elimu ya juu.

Katika taarifa yake, Dk Kawambwa alisema kuwa mfano mzuri ni mwaka huu wa masomo 2012/13 ambao kati ya wanafunzi 45,788 walioomba mikopo, ni 30,144 tu ndiyo waliopata na katika mchujo, wengi wao walibainika kuwa na uwezo mdogo wa kuchangia elimu hiyo ya juu.

Dk Kawambwa alisema asilimia 72.17 ya waliopangiwa mikopo kwa kipindi cha 2012/13 wana uwezo wa kuchangia chini ya Sh500,000.

Alisema idadi ya wanafunzi wanaokopeshwa na Bodi ya Mikopo kwa mwaka, imeongezeka kutoka 42,729 mwaka 2005/6 hadi kufikia 93,149 mwaka 2011/12 wakati fedha za ukopeshaji zimeongezeka kutoka Sh56.1 bil mwaka 2005/6 hadi kufikia Sh326 bilioni mwaka 2012/13.

Dk Kawambwa alisema hadi kufikia mwaka wa masomo wa 2011/12, wanafunzi 154,519 na jumla ya Sh1,133,386,869,067.58 zimeshatolewa.
Alisema pia kuanzia Juni 1994 na Juni 2012 wanafunzi 203,149 wamepata mikopo na fedha zilizotolewa ni sh1,184,490,554,983.58.

Alisema Sh160,730,886,339 za mikopo iliyoiva ni Sh43,558,020,863.33 zilizopaswa kurejeshwa ilhali zilizorejeshwa ni Sh28,010,000,000.43.

“Mkakati uliopo wa kuhakikisha mikopo inarejeshwa ni kuwaelimisha wadaiwa, waajiri, kutuma taarifa za watumishi walioajiriwa serikalini kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuwatambua wadaiwa mahali walipo na kuwatumia mawakala.

Tume ya kuinusuru
Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali iliunda kamati mbalimbali zilizoshauri juu ya kuwa na mfumo endelevu kugharimia elimu ya juu, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfuko wa dhamana.

Akizungumzia mapendekezo ya uchangiaji kupitia mifuko ya jamii, Dk Kawambwa alitaka mifuko ya hifadhi ya jamii ibuni na kutoa kwa wanachama wao fao la elimu ya juu au mikopo kwa faida ya wanachama na watu wengine.

Kuhusu taasisi za kifedha, alitaka zitenge fungu kwa ajili ya kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu kwa kuzingatia masharti ambayo hayataathiri uendelevu wa fungu.

Katika hoja yake, Nchemba alisema sheria zilizopo haziwabani wanaokopa kurudisha mikopo kwa utaratibu uliopangwa na kusema kuna haja ya kuziangalia upya sheria hizo.
Alisema kuna haja ya kuweka riba katika mikopo kwa waliokopa na kushindwa kurudisha kwa wakati.

Previous Post Next Post

Popular Items