SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), imeondoa ombi la dharura la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 155 lililoliwasilisha Januari Mosi, mwaka jana kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu alisema Novemba 9, 2011 Ewura ilipokea ombi la dharula kwa Tanesco lililohusu marekebisho ya bei za umeme ikiomba nyongeza ya wastani wa asilimia 155 kuanzia Januari Mosi, 2012.
Masebu alisema Ewura kwa kuzingatia uchambuzi wa awali, ilitoa agizo la kuidhinisha bei ya dharura ya umeme kwa nyongeza ya asilimia 40.9 ambazo zimeendelea kutumika mpaka Januari 31, mwaka huku huku ikiendelea kutathmini ongezeko hilo walilohitaji. Alisema kabla mchakato wa kukokotoa bei haujakamilika, Tanesco kupitia barua yake ya Januari 14, mwaka huu iliondoa maombi yake ya ongezeko la bei.
Awali, kabla ya uamuzi wa Tanesco, Ewura iliajiri mtaalamu mwekeleza wa kujitegemea kutoka Hispania kufanya uchambuzi wa gharama za kutoa huduma ya umeme kwa Tanesco, alitoa mapendekezo ya bei za umeme kwa miaka mitatu.
“Taarifa ya mtaalamu elekeza ilipendekeza nyongeza ya bei ya za umeme kwa asilimia 33.8 kwa mwaka huu, ikifuatiwa na ongezeko dogo la asilimia 0.85 kwa mwaka 2014 na asilimia 15.14 kwa mwaka 2015,” alisema Masebu.
Alisema kwa mujibu wa kanuni namba 19(2)(b) ya sheria namba namba 414, Ewura ilifanya taftishi kukusanya maoni ya wadau juu ya uhalali wa bei zilizopendekezwa na mtaalamu mwelekezaji. Alisema Desemba 10, mwaka jana Ewura ilifanya mkutano wa wadau na Januari 2, mwaka huu lakini kabla mchakato wa kukokotoa bei kukamilika Tanesco iliondoka maombi yake.