Wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, klabu ya Azam fc wana lambalamba leo hii wamewabamiza bila huruma Africa Lyon mabao 3-1, katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara uliopigwa leo hii dimba la Chamazi Complex maeneo ya Mbande nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mabao ya Azam fc yametiwa kambani na wachezaji Khamis Mcha “Vialli” dakika ya 12, huku nyota wa klabu hiyo kutoka Pwani ya magharibi mwa Afrika, nchi ya Ivory coast, Kipre Herman Tchetche akikwamisha kimiani mabao mawili katika dakika ya 31 na 61 ya mchezo huo.
Bao pekee la kufutia machozi kwa upande wa Africa Lyon wanaohitaji kukwepa mkasi wa kushuka daraja limewekwa kimiani na Adam Kingwande dakika ya 37 kipindi cha kwanza.
Akizungumza muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Afisa habari wa Azam fc, Jafar Idd Maganga amesema wamefurahi kupata ushindi mnono mbele ya wapinzani wao ambao wanajitahidi kufanya vizuri ngwe hii ya lala salama ili wasalie ligi kuu msimu ujao.
“Kipindi cha kwanza kiukweli Lyon walitulia na kucheza vizuri, lakini kipindi cha pili tuliwazidi sana na tumewashinda kwa halali, sasa hesabu zetu ni mnyama Simba ambaye tunakumbana naye mwishoni mwa wiki hii”. Alisema Idd.
Idd alisema baada ya kuibuka na ushindi leo hii wamefikisha pointi 46 wakizidiwa na Yanga pointi 3 walioko kileleni kwa kujikusanyia pointi 49 ingawa Azam wao wamecheza mechi moja zaidi, wao wanajipanga kushinda kila mchezo uliosalia wakianza na wekundu wa msimbazi Simba walioweka rehani ubingwa wao msimu huu.
“Si kazi nyepesi, kila mtu amejipanga barabara dakika hizi za lala salama, lakini tuna timu nzuri inayoweza kushindana, sasa kocha wetu anajipanga upya kwa ajili ya Simba ambayo imejaza vijana waliotufunga siku za nyuma”. Aliongeza Idd.
Wakati hayo yakijili kwa Azam fc, wapinzani wao Africa Lyon wamekiri kupoteza kihalali mchezo huo kwani walizidiwa umakini na wenyeji wao.
Katibu mkuu wa klabu hiyo Ernest Brown amesema walipata nafasi za kufunga, lakini safu yao ya ushambuliaji ni butu sana na ndio maana walishindwa kutumia mtaji huo.
“Nafikiri walichotuzidi wapinzani wetu ni kucheza na nafasi, walitumia vyema makosa yetu na kuvuna mabao matatu yaliyowapa pointi tatu muhimu, lakini tunajipanga kwa michezo ijayo, hakika hatuna cha kujutia, ni kusonga mbele. Aliongeza Brown.
Akizungumzia kitendo cha kocha wao mkuu Mkenya Charles Otieno kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo, Brown alisema kitebdo hicho kimetokea kutokana na wawili hao kutoelewana.
“Otieno alitaka kuzungumza na mwamzi, kilichotakiwa ni busara za mwamzi, soka sio vita hata siku moja, angemsikiliza wangeelewana, lakini kumtoa benchi yalikuwa maamzi ya haraka sana”. Alisema Brown.
Katibu huyo alisisitiza kuwa kutolewa kwa kocha wao hakukuathiri mchezo huo kwani wachezaji wao waliendelea kupambana japokuwa walizidiwa na wapinzania wao ambao kwa sasa wako vizuri zaidi ya Lyon.
Baada ya michezo hiyo, mwishoni mwa wiki yaani Jumamosi, Vinara wa ligi hiyo Yanga ya Dar es Salaam wataumana na JKT Oljoro, wakati jumapili mabingwa wa zamani wa Tanzania, Coastal unioni ya Tanga watakuwa na kibarua kizito mbele ya wekundu wa msimbazi simba uwanja wa taifa.
VIKOSI:
Azam: Aishi Salum, Himidi Mao, Waziri Salum, Jockins Atudo, Luckson Kakolaki, Jabir Aziz, Kipre Tchetche, Ibrahim Mwaipopo, Abdi Kassim, Salum Abubakar, Mcha Khamisi
African Lyon: Noel Lucas, Ibrahim Isaac, Sunday Bakari, Yussuf Mlipili, Obinna Salamusasa, Juma Seif, Jackob Massawe, Mohamed Samatta, Adam Kingwande, Freddy Lewis, Ndela Kashakala