Dk Nchimbi alisema timu ya wataalamu ipo Mtwara kuweka mambo sawa na kusema Serikali itatimiza majukumu yake pasi na shaka yoyote na kusisitiza kuwa haiwezi kukubali Tanzania ikawa vipande.
Alisema Serikali inafanya tathmini kujua hali ilivyo Mtwara na ikibidi itasitisha shughuli zote za kisiasa mkoani humo.
Mtwara wampinga
Wakazi wa Mkoa wa Mtwara wamegawanyika baada ya ziara ya Waziri Mkuu baada ya baadhi yao kupinga mpango wa Serikali wa kusafirisha gesi asilia kwa bomba kwenda Dar es Salaam.
Katika ziara yake, Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya manufaa yatakayopatikana mkoani Mtwara kutokana na uzalishaji wa nishati hiyo kiasi cha kumshangilia na kumpigia makofi.
Shura ya Maimamu Mtwara imesema jana kwamba haijaridhishwa na majibu iliyoyaita mepesi ya Waziri Mkuu katika hoja nzito na kwamba bado Serikali haijaupatia suluhu mgogoro huo.
“Baada ya kutoka pale tulifanya kikao kupitia maelezo ya Waziri Mkuu, kuna maeneo hatujaridhika … amezungumzia ‘powerplant’ (mtambo wa kufua umeme) kama mtambo wa kusafisha gesi, ndiyo aliousema utajengwa Madimba… lakini sisi tunahitaji ‘powerplant’, mashine za kufua umeme pamoja na hiyo ya kuchakata gesi iwe Mtwara… katika eneo hilo hatujaridhika,” Msemaji wa Shura hiyo, Sheikh Abubakar Mbuki alisema na kuongeza:
“Waziri Mkuu asituambie tu gharama za kutandaza nyaya ni kubwa kuliko bomba la gesi akaishia hapo. Atuambie gharama hizo ni kiasi gani badala ya kusema ni gharama kubwa… mbona gharama za bomba zipo wazi, kwa nini hizi za nyaya hazisemwi?”
Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Katani Katani alisema “Sijaelewa kabisa… nashangaa watu wanashangilia wakati madai yetu ya msingi hayajapata ufumbuzi… dai letu la kwanza lilikuwa viwanda vya kuchakata gesi vijengwe Mtwara, hilo limepatiwa ufumbuzi, la pili lilikuwa mitambo ya kufua umeme Megawati 600 ijengwe Mtwara.”
“Hili hajalipatia ufumbuzi, tunachokataa sisi wana Mtwara ni kusafirisha gesi kwa njia ya bomba, tunataka mashine zinazojengwa Kinyerezi zihamishiwe Mtwara… kutuambia kupeleka umeme Dar es Salaam kwa njia ya nyaya ni gharama kubwa hilo sikubaliani.”
Alisema kutokana na kutopatikana kwa ufumbuzi wa dai hilo moja, bado wananchi wa Mtwara wataendelea kupinga mradi huo.
Akizungumza katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake juzi, Pinda alisema gesi ghafi haitasafirishwa kwa bomba kwenda Dar es Salaam na badala yake usindikaji utafanyika Mtwara.
“Wataalamu wanasema gesi haiwezi kwa namna yeyote ile kusafirishwa kama ilivyo, lazima ibadilishwe kuwa hewa au barafu… kiwanda cha kusafisha gesi kitajengwa Madimba, gesi yote itakayotoka Mnazi Bay itasafishwa hapo na masalia yote yatabaki huku ili kuvutia viwanda vya mbolea na vingine vinavyotumia malighafi hizo,” alisema Pinda na kuongeza:
“Kama tungekuwa tunasafirisha gesi ghafi basi hata kiwanda cha Dangote kisingejengwa hapa… gesi itakayopelekwa Dar es Salaam ni ile iliyosafishwa kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme… tusaidieni wenzetu kuliokoa Taifa na tatizo la umeme.”