SALAMU ZA RAMBI RAMBI MSIBA WA SAJUKI


 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI,UTAMADUNI NA MICHEZO
 
logo tanzania.jpg
Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara amewatumia salamu za rambirambi, ndugu, jamaa na wasanii wote nchini kufuatia kifo cha msanii Juma Kilowoko (SAJUKI)kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Taarifa iliyotolewa leo, jijini Dar es salaam ,Wizara ya Habari, Vijana na Utamauni na Michezo imepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha msanii huyo na kuongeza kuwa kifo hicho ni pigo katika tasnia ya filamu hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Kifo chake ni pengo kubwa kwa Serikali, wadau wa tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza nchini kwa ujumla.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha SAJUKI sina maneno ya kuelezea masikitiko na huzuni nilinayo , kwani kifo chake ni pigo katika tasnia ya filamu za michezo ya kuigiza” alisema Dkt Mukangara.

Dkt. Mukungara amewataka ndugu, jamii na wasanii wote kuwa wavumilivu na watumilivu wakati wote wa msiba na kumuombea marehemu makao mema kwa Mwenyezi Mungu.

Juma Kilowoko (SAJUKI)ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma. Sajuki alianza kujihusisha na masuala ya maigizo alipojiunga na kikundi cha Kaole na baadaye filamu. Filamu alizocheza ni pamoja na Revenge ya Kampuni ya RJ .

Mwaka 2008 aliamua kuanza kutengeneza kazi zake mwenyewe ambapo filamu yake ya kwanza iitwayo Two Brothers kwa kushirikiana na Shija Deogratious ilitoka. Sajuki baadaye aliamua kuanzisha kampuni yake iitwayo WAJEY Production Company ambapo alitengeneza filamu nyingi zikiwemo Mboni Yangu, Round, Briefcase , Kijacho, Kozopata, Mchanga na Keni, 077( Zero Seven Seven).nk.

Sajuki alifanikiwa kucheza michezo ya kuigiza na filamu na wasanii wengi wenye majina hapa nchini. Sajuki amebobea katika Uigizaji, Utayarishaji na Uongozaji wa filamu.

Sajuki alianza kuugua mwaka 2010 na hali ilizidi kudhoofu mwaka 2011,ambapo alikwenda kutibiwa nchini India. Wadau wengi wa tasnia ya filamu walifanikiwa kutoa michango mbalimbali iliyomwezesha Sajuki kupata matibabu yake. Alirudi na kuonekana kapata nafuu kidogo jambo ambalo lilileta matumaini na furaha kwa watanzania; aliporejea tu aliweza kutoa filamu iitwayo Kivuli huku filamu nyingine ikiwa katika hatua ya utengenezaji.

Aidha hali yake ilibadilika jambo lililolazimu alazwe katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili hadi umauti ulipomkuta usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013.

Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi Amen.

Imetolewa na: 
Mkurugenzi 
Idara ya Habari(MAELEZO). 
Dar es Salaam. 
2 Januari 2013
**********

Yah: Salaam za Rambirambi
Baraza la Sanaa la Taifa limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii wa tasnia ya filamu nchini Sadick Juma Kilowoko a.k.a Sajuki.

“ Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Sajuki ambaye mchango wake unahitajika sana katika tasnia ya sanaa, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wao bado unahitajika katika tasnia hii.” Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha linawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.

Tunaomba mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, tutambue kuwa haya ni mapenzi ya Mungu.


Imetolewa na
Ghonche Materego
Katibu Mtendaji
Baraza la Sanaa la taifa.
Previous Post Next Post