Lulu aachiwa kwa dhamana

Mahakama Kuu ya Tanzania mchana huu imeweka wazi masharti ya dhamana ya msanii wa filamu anayejulikana zaidi kwa jina la Lulu,. Lulu ambaye jina lake halisi ni Elizabeth Michael anakabiliwa na mashtaka ya kuua bila kukusudia ya msanii mwenzake(ambaye inasemekana walikuwa na mahusiano ya kimapenzi), Steven Charles Kanumba, kilichotokea April mwaka jana huko Sinza-Vatican jijini Dar-es-salaam.




Kwa mujibu wa chanzo chetu kilichokuwepo mahakamani mchana huu, dhamana ya mwigizaji Lulu ipo wazi endapo tu atatimiza masharti aliyotengewa ambayo ni

  • Kuwasilisha au kukabidhi hati yake ya kusafiria(passport) 
  • Kutosafiri nje ya Dar es salaam. 
  • Kuripoti mahakamani kila siku ya kwanza ya kila mwezi 
  • Kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atamdhamini kwa shilingi milioni 20 za kitanzania. 


Pamoja na kwamba familia ya Lulu walikuwa wameshajiandaa kukabiliana na kutimiza masharti hayo, Lulu amerudi rumande leo kutokana na kwamba watumishi wawili wa serikali(Mahakama) ambao wanahusika na sehemu ya dhamana hiyo kwa upande wa sahihi za kimahakama, hawakuwepo Mahakamani hapo kutokana na kuwa safarini mkoani Pwani kikazi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mawakili wanaomwakilisha Lulu, masharti yote ya dhamana wameshayatimiza na kinachosubiriwa ni huo uthibitisho na utaratibu wa kimahakama ili Lulu arejee nyumbani na kuendelea kukabiliana na kesi hiyo akiwa uraiani.

Kwa maana hiyo, uwezekano ni wazi kabisa kwamba Lulu ataachiwa rasmi kesho January 29, 2013.

Previous Post Next Post