MGHANA WA SIMBA AITAMANI TAIFA STARS

MSHAMBULIAJI wa Simba, Daniel Akuffor amesema kuwa  anatamani apewe uraia wa Tanzania ili avae jezi ya timu ya taifa Taifa Stars.

Akuffor raia wa Ghana amecheza mechi mbili za kirafiki akiwa na Simba dhidi ya Mathare United na Oljoro JKT na kufunga kila mchezo katika dakika 50 alizocheza.

Mchezaji huyo alisema jana mjini Arusha kwamba anatamani kuvaa jezi ya Taifa Stars na ana uhakika wa kupiga mabao kama kawaida.

"Ninatamani sana kuichezea Tanzania kwa vile ni sehemu nzuri, ina mazingira mazuri ya kucheza soka, ninaweza kufanya kazi kubwa sana nikiwa na Simba pamoja na Taifa Stars,"alisema Akuffor.

Alisema,"unajua mchezaji kufanikiwa unahitaji mazingira tulivu na  watu wanaojali mpira, nikipata nafasi hiyo nitafanya kazi. Nimechezea Ghana ya U-17 mwaka 2005 na ukiangalia timu ya wakubwa kwa sasa ina ushindani mkubwa sana na wachezaji wengi wanaoichezea wanacheza soka Ulaya."

Akuffor alisema,"kama nikipewa nafasi Taifa Stars nitafanya kazi, nipo tayari kuuvua uraia wa Ghana, haimaanishi kwamba Ghana hakuna amani, lakini nikipata nafasi Tanzania nitafanya kazi Simba na timu ya Taifa Stars."

Mchezaji huyo hivi sasa amekuwa kipenzi na mashabiki wa soka jijini Arusha kutokana na wepesi wake na jinsi anavyoichangamsha safu ya ushambuliaji ya Simba.

Simba imepiga kambi jijini Arusha, ambapo itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya City Stars ya Kenya siku ya Jumapili.

Wakati huo huo; Simba imefuta safari ya kwenda Tanga baada ya Yanga kuichukua Coastal Union na kuificha Dar es Salaam.

Wekundu hao walikuwa wamepanga kwenda Tanga siku ya Ijumaa na kucheza Jumamosi na Coastal kabla ya kuweka kambi ya muda mpaka Jumatano.

Lakini uongozi umefuta safari hiyo na sasa Simba itaendelea na kambi jijini Arusha mpaka Jumatano timu itakaporudi Dar es Salaam kujiandaa na mechi dhidi ya Azam ya ngao ya hisani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba, Ibrahim Masoud alisema jana kuwa wameamua kubaki Arusha na watacheza mechi zote za kirafiki katika jiji hilo.

"Tumebaki hapa kutokana na hali ya hewa ya baridi ambayo ni nzuri kwetu, kwa vile wachezaji wakifanyia mazoezi kwenye mazingira kama haya halafu tukaenda kucheza kwenye joto Dar es Salaam itakuwa nzuri sana kwetu,"alisema Masoud.

Lakini habari za ndani ya kambi ya Simba kwenye hoteli ya Briston zinasema wameahirisha safari hiyo ya Tanga baada ya Yanga kuing'ang'ania Coastal na kuipeleka Dar es Salaam kucheza nayo Jumamosi.

Habari zinasema Simba ilipanga kucheza nao mechi mbili za kirafiki na kuzoea hali ya hewa ya joto kabla ya kurudi Dar es Salaam.

Previous Post Next Post