Koffi Olomide akamatwa na polisi kwa kujiita ‘Old Ebola’

Mwanamuziki maarufu wa Jamhuri wa Kidemokrasi ya Kongo, Koffi Olomide alikamatwa na polisi na kuhojiwa kutokana na kujiita ‘Old Ebola’ (Vieux Ebola) kwenye matangazo ya show yake ijayo.



Kwa mujibu wa rafiki yake wa karibu, jina hilo amepewa na mashabiki wake na kwamba hawana uwezo wa kuwazuia. Koffi Olomide alilazimika kutoa maelezo kwa polisi nchini humo.

“Imebidi kufuatilia kwasababu tupo kwenye vita dhidi ya mlipuko wa Ebola. Ni ujumbe mbaya unaotangazwa,” alisema Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa polisi Colonel Pierrot Mwana-Mputu.

“Ebola, inamaanisha kifo. Ni kama tunapingana na jitihada za jumuiya ya kimataifa kupambana na ugonjwa huo,” alisema.

Polisi waliamuru kuondolewa kwa mabango hayo katika mjini wa Kinshasa. Tayari mwanamuziki huyo ameachiwa.

Hiyo sio mara ya kwanza muimbaji huyo kujipa majina ya utani yaliyosababisha mzozo. Majina mengine aliyowahi kutumia zamani ni ‘Sarkozy’ na ‘Benedict XVI ambapo kanisa katoliki lilimzuia kutumia jina hilo.

Hata hivyo imebainika kuwa Koffie anajiita ‘Old Ebola’ kama vita aliyoanzisha dhidi ya JB Mpiana ambaye wamekuwa na uadui.
Previous Post Next Post