Baada ya kutolewa kwenye KTMAs, Madee adai BASATA wamechelewa

Habari ya kuondolewa kwa wimbo wa Madee ‘Tema Mate’ kwenye kinyang’anyiro cha KTMAs bila shaka zimewasikitisha wanafamilia wa Tip Top Connection na mashabiki walioipendekeza kwa kura nyingi ngoma hiyo.

Kwa upande wa Madee ameiambia tovuti ya Times Fm kuwa BASATA wamechelewa katika kuchukua uamuzi huo kwa kuwa wimbo ulitoka zamani na kushika nafasi ya kwanza kwenye chart nyingi za radio.



“Mimi nahisi walikuwa wamechelewa ndio maana kila siku nalilia kwamba kuwe kuna chombo ambacho muziki wetu tukishamaliza kuutengeneza tunapitisha pale then wanasikiliza kama inafaaa kwenda hewani inafaa kama haifai tunaaambiwa mapema. Lakini chombo hicho hakuna, kwa hiyo wanakuwa kama wanafake kwa sababu mwisho wa siku wimbo unakuwa unasambaa na watu wanakuwa wameshaipenda.” Amesema Madee.

Ameeleza kuwa kutokana na kuchelewa huko watangazaji wa radio na Television ambao wanakuwa wanacheza wimbo huo na kuuweka kwenye chart kama namba moja, pale unapozuiwa nao wanaonekana kama hawana maadili bora.

Rapper huyo wa Manzese ameeleza kuwa hafahamu hasa kwa nini wimbo huo umeonekana hauna maadili wakati yeye alijua mara ya kwanza kuwa video ya wimbo huo ndiyo iliyokuwa imetajwa kuwa kinyume na maadili.

Hata hivyo, Madee amesema tangu aanze muziki miaka 14 iliyopita hajawahi kupata tuzo ya Kili hivyo haoni hasara yoyote kwa kuondolewa kwenye kinyanyiro hicho.

“Nimeshazoea yaani haitoniaffect chochote na wala haitakuwa na hasara yoyote kwenye muziki wangu, zaidi tu ni kuwashukuru wale ambao walisapoti muziki wangu ukafika huko mpaka watu wakakaa leo kuijadili, wamepoteza dakika zao kadhaa kuijadili kwa hiyo ni kawaida mimi sioni kama nitaathirika na chochote.” Madee ameongeza.

Tovuti ya Times Fm ilimtafuta kaimu katibu mtendaji wa BASATA, Godfrey Mnengereza na kumuuliza mtazamo wake na BASATA kuhusu alichokisema Madee.

“Nimependa sana maoni ya Madee, kumbe tuko pamoja kwamba hazungumzii kwamba wimbo wake haukidhi hivyo vigezo. Anazungumzia na anatoa ushauri kwa baraza kwamba tumechelewa kwa sababu wimbo umepigwa mwaka mzima na kwamba tufanye censorship. Kwa sasa hivi ni kweli ninakubali kabisa kwamba si sahihi sana wimbo uende hewani ndipo tuanze kuzuia.” Amesema Godfrey Mnengereza.

“Kwa upande wa tuzo mchakato wake ndio umeenza sasa na tunaangalia kazi zilizopita. Lakini nimeshukuru sana kwa ushauri wake kwamba tuweze kufanya censorship, na ndiko tunakoelekea kwamba katika suala zima la urasimishaji kazi yoyote ya muziki wa audio inabidi ipite baraza, sasa ni kwamba tu ni kitu bado kigeni. Lakini vile vile tunatakiwa tushirikiane na vyombo vya habari kwamba wasiruhusu kazi ambazo zinamdhalilisha msanii mwenyewe, au zina matusi ndani yake au zina lugha ya uchochezi.” Kaimu Katibu mtendaji wa BASATA ameileza tovuti ya Times Fm.

Mbali na wimbo wa Madee ‘Tema Mate’, nyimbo nyingine zilizoondolewa kwenye KTMAs kwa madai ya kukiuka maadili ni Uzuri Wako ya Jux, na Nimevugwa ya Snura.
Previous Post Next Post