WABUNGE 15 MATATANI NI BAADA YA KUCHUKUA POSHO ZA SAFARI BILA KUSAFIRI UKU WENGINE...

Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limewaanika wabunge 15, waliobainika kuchukua posho za safari bila kusafiri huku wengine wakikatisha safari zao. (HM)


Akizungumza katika mahojiano maalumu jana na mwandishi wa gazeti hili, Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah, alisema tayari fedha hizo zimesharejeshwa kwa kukatwa kwenye mishahara yao.

Dk Kashililah alisema baadhi ya wabunge waliomba wasikatwe fedha hizo kwenye mishahara yao, badala yake wazirejeshe wao wenyewe.


Hata hivyo, Katibu huyo wa Bunge alisema wabunge hao walishindwa kusafiri kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo kuwa na ugeni wa viongozi wa chama na matatizo ya kifamilia.
"Kwa mfano Komba (Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba) alishindwa kwenda kwa sababu ya kutembelewa na ziara ya Katibu wake wa Chama (Abdulrahman Kinana) muda wa safari ukamalizika hivyo akashindwa
kusafiri na taarifa zilikuwepo ofisini," alisema Dk Kashililah na kuongeza.
Akizungumzia safari ya Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani, Freeman Mbowe nchini Uingereza, Dk Kashililah alisema Bunge halina uwezo wa kumzuia mbunge yeyote kufanya shughuli zake safarini baada ya kumaliza jukumu lililompeleka.
Dk Kashililah alisema Mbowe alikamilisha ziara yake ya Bunge na kwamba baada ya hapo aliendelea na shughuli za chama chake nchini humo.
"Suala hili lilikuwa limebeba hisia za kisiasa, baada ya kusikika tu bungeni basi vyombo vya habari vikaanza kuwahukumu wabunge ni mafisadi bila hata kutafuta ufafanuzi kutoka wetu. Sisi taarifa hizo tulikuwa nazo kabla ya hata ya kuibuka bungeni, lakini lilivyotafsiriwa sikupenda," alisema Dk Kashililah.
Dk Kashililahb alisema, "Bunge lilikuwa limeratibu jumla ya safari mbalimbali zilizokuwa zimependekezwa na Kamati 16, lakini hazikufanikiwa kwenda zote kwa pamoja.
Alisema ziara zote za kamati huandaliwa kwa mujibu wa kanuni ya 117 ambayo inazipatia mamlaka Kamati hizo kuandaa ziara inazooana zina manufaa kwa ajili ya kuboresha utendaji wake. 

Chanzo: mwananchi


Previous Post Next Post