HATIMAYE Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameweka wazi mshahara wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Zitto ameutaja mshahara huo wa Pinda anayejitambulisha kama ‘mtoto wa mkulima’ juzi mjini Mpanda na jana wilayani Sikonge wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika ziara ya Kanda ya Magharibi kwa ajili ya ujenzi wa chama.
Alisema Pinda anapokea jumla ya sh milioni 26, ambazo ni kiasi kikubwa kulinganisha na uchumi wa nchi.
Akichanganua alisema Pinda anapokea sh mil. 11.2 kama mbunge, sh mil. 8 kwa nafasi ya waziri na kiasi kinachosalia kufikia sh mil. 26 kwa nafasi yake ya uwaziri mkuu.
Alisema sababu hiyo ya mishahara mikubwa isiyokatwa kodi ndiyo huwafanya viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wakali pale vyombo vya habari vinapotaka kuwafahamisha wananchi namna watumishi wao wanavyojilipa.
“Nimeanza na mshahara wa waziri mkuu pia siku zijazo nitataja na wa rais, kwa kuwa amesaini makubaliano na Serikali ya Marekani kuendesha nchi kwa uwazi, na moja ya uwazi ni kwa muajiri kujua kiasi anachomlipa mwajiriwa wake,” alisema Zitto.
Hatua ya Zitto imekuja baada ya kuwapo mvutano mkubwa kuhusiana na kile kinachodaiwa ‘usiri’ wa mishahara ya watumishi wa umma, wakati ni haki ya walipa kodi kujua kile wanachowalipa walioomba kuwaongoza.
Kodi ya laini za simu
Akizungumzia sakata la kodi katika laini za simu, Zitto alisema CCM ina ajenda ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Alisema serikali baada ya kubaini watu wengi wanapeana taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi, hususan katika masuala ya kisiasa, wakaona njia sahihi ya kudhibiti ni kuwatoza kodi ya laini ili kupunguza hatari ya mawasiliano hayo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.
“Sikuwepo bungeni wakati wabunge wa CCM wanapitisha kadhia hiyo ya kuwanyonya wananchi, wenzangu wakaniambai tukasema hapana, kwa maana tuliona hii leo kuna Watanzania wengi wasio na uwezo wa kuhudumia simu kwa kiasi cha sh 1,000 kwa mwezi,” alisema Zitto.
Akijibu maswali ya wananchi mjini Mpanda waliotaka kujua sababu ya kupunguza makali bungeni, Zitto alisema hakuna makali yaliyopungua bali ni mitazamo ya watu.
Alisema kwa kushirikiana na wabunge wenzake wa upinzani wamekuwa wakisimamia hoja zenye manufaa kwa wananachi huku wabunge wanaojipambanua kuwa majasiri kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwaunga mkono wazi wazi.
Akiwa wilayani Sikonge, Zitto alisema Watanzania hawawezi kujivunia uhuru huku mama zao, watoto wao na wazee wao wakiwa hawana uhakika wa kupata huduma bora ya afya, elimu na maji safi.
Alisema kwa sasa Tanzania ni taifa moja lililogawanyika katika nchi mbili za wenye fedha na wasio na fedha.
Alisema nchi ya wenye fedha, familia zao husoma katika shule bora, zenye mazingira bora na walimu wazuri, hutibiwa katika hospitali zenye hadhi na huduma muhimu na ikibidi nje ya nchi, huku nchi ya wasio na fedha familia zao wakiishi kwa shida, kusoma katika majengo ya shule na walimu wasiopata mishahara ya kuridhisha na hospitali zisizokuwa na huduma muhimu licha ya kuchangia kiasi cha fedha kwa ajili ya bima ya afya.
Source:Tanzania Daima