WIZI WA NYAYA ZA MKONGO WA TAIFA

nyaya 2764b
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unakabiliwa na hujuma kubwa na tayari jumla ya mita 4050 za nyaya, zimeibwa.
Kitendo hicho kimesababisha maeneo mbalimbali yakiwemo ya Uwanja wa Ndege Mwanza, kukosa mawasiliano.
Akizungumza katika hafla ya kuwashukuru wateja wao ,Meneja wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) mkoani Mwanza, John Kalisa, alisema hujuma hizo zimefanyika katika katika kipindi cha kati ya Januari mwaka jana na Aprili mwaka huu.
Kwa mujibu wa meneja huyo, hatua hiyo imesababisha hasara ya Sh800 milioni.

Kalisa alisema wizi huo umeathiri utoaji wa huduma za simu za TTCL na wateja wake.
Alisema maeneo yaliyokithiri kwa hujuma hizo na kiasi cha nyaya zilizoibwa kikiwa katika mabano ni, Uwanja wa Ndege (mita 1600), Nyakato (mita 300), Nyakato Viwandani (mita 450) na Igogo Viwandani (mita 800).
Maeneo mengine ni Nyakato-Mwananchi (mita 150) Geita (mita350) na Magu ( mita 400).
"Wizi huo umegawanyika mara mbili, kuna wanaoiba wanya ndogo ambazo imebainika kuwa wamekuwa wakizitumia kujiunganishia umeme majumbani, na wizi mwingine ni ule unaohusu nyaya kubwa za mkongo ambazo huuzwa," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, alisema hujuma hizo zinasababisha hasara kubwa kwa taifa.
Alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, atazishughulikia kwa umakini.
Aliviagiza vyombo vya usalama kuchukua hatua dhiudi ya watakaobainika.
Alisema TTCL ndiyo muhimili wa mawasiliano hapa nchini na kwamba hujuma zitandelea, hali ya mawasiliano itaathirika.Kwa upande wake, Ofisa Mauzo na Masoko wa TTCL, Peter Ngota, alisema kwa sasa wizi huo umekuwa ukikwamisha jitihada za kampuni yake kutoa huduma kwa wananchi mkoani Mwanza.

CHANZO: MWANANCHI.
Previous Post Next Post