Nchi za magharibi zinatarajiwa kuongeza shinikizo la kupitishwa kwa azimio la umoja wa Mataifa kuishurutisha Syria kuzisalimisha silaha zake za sumu baada ya umoja wa Mataifa kuripoti sarin ilitumika Syria
Umoja wa Mataifa hapo jana bila ya kuulamumu upande wowote katika vita vya Syria ulisema umekusanya ushahidi wa kutosha na wa kuaminika unaoonyesha kuwa sumu ya sarin ilitumika katika shambulio la Ghouta viungani mwa mji mkuu wa Syria Damascus mwezi uliopita.(P.T)
Marekani imekuwa ikiulaumu utawala wa Syria kwa shambulio hilo lililowaua kiasi ya watu 1,400 na kusema lawama inamuangukia kikamilifu rais Bashar al Assad.
Mjumbe wa Marekani katika umoja wa Mataifa Samantha Power amesema matokeo ya uchunguzi huo wa umoja wa mataifa unadhihirisha wazi kuwa ni utawala wa Syria tu ungeweza kufanya shambulio la kiwango kikubwa hivyo cha sumu.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza na Ufaransa pia wamesema hakuna shaka yoyote kuwa serikali ya Syria ndiyo ingeweza kufanya shambulio la namna hiyo baada ya ushahidi huo uliotolewa hapo jana.
Silaha za sumu sharti ziangamizwe
Mjini Berlin waziri wa mambo ya nchi za wa Ujerumani Guido Westerwelle alisema hivi sasa uafafanuzi umepatika na kwamba Ulimwengu unajukumu kubwa zaidi la kuweka wazi na kwamba mauaji ya raia kwa kutumia silaha za sumu si jambo litakalokubalika hata kidogo.
Westerwelle alisema hivi sasa hakuna wakati wa kupoteza ni lazima wataalamu wa Umoja wa mataifa waanze kazi ya kuutekeleza mpango wa kuziangamiza silaha za sumu za Syria na wakati huo huo lazima jamii ya kimataifa kuushinikiza utawala wa Assad utowe ushirikiano wa kutosha katika suala hilo.
Wakati huo huo Syria imezishutumu nchi za magharibi kwa kujaribu kulazimisha ajenda zao kwa watu wa Syria na kuunga mkono makundi ya kijihadi . Matamshi hayo yalitolewa baada ya nchi hizo kusema zitashurutisha azimio la kuibinya Syria.
Ufaransa na Uingereza hivi karibuni zitawasilisha rasimu ya azimio kwa wanachama wengine wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa zikitaka Assad kuwekewa vikwazo iwapo atakiuka mpango wa kuzisalimisha silaha na shambulio hilo la silaha za sumu kuwasilishwa katika mahakama ya kimataifa kushughulikia uhalifu.Baraza hilo linatarajiwa kuanza vikao vyake wiki hii.
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban ki Moon amelaani matumizi ya silaha za sumu nchini Syria na kuyataja uhalifu wa kivita na kuwa inashutusha kusoma ripoti hiyo kutoka kwa wachunguzi.
Wachunguzi wa silaha za sumu wa umoja wa Mataifa nchini Syria
China imesema itadurusu kwa makini ripoti hiyo ya umoja wa Mataifa ili kujua kwa undani yaliyomo kwenye hiyo ripoti.Urusi kwa upande wake imesema uchunguzi zaidi unapaswa kuendeshwa kuhusu matumizi ya silaha za sumu Syria.
Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters/ap
Via Mjengwa
Tags:
Social