SIMBA SC YAIFUNGA KMKM MAGOLI 2-1


simba-sport-club-ngassa_71be4.jpg
WEKUNDU wa Msimbazi Simba SC, Chini ya kocha wake Abdallah Kibadeni "King Mputa" , kwa mara nyingine tena wamewatambia Wazanzibar baada ya kuwazamisha mabao 2-1 mabingwa wa Zanzibar KMKM katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jioni ya leo dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa katika dakika ya 28 na nyota wake Said Ndemla baada ya kupokea pande maridadi kutoka kwa Issa Rashid "Baba Ubaya"
Mnyama alitinga tena nyavuni katika dakika ya 41 baada ya beki wake, Mrundi, Gilbert Kaze kupiga shuti la moja kwa moja kufuatia kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga chenga ama kupiga rangi mpira, Ramadhan Chombo "Redondo wa Kibongo" kufanyiwa madhambi.
KMKM chini yakocha wake, Ally Bushiri ilipata bao lake la kusawazisha katika dakika ya 54 kupitia kwa Iddi Kambi aliyetumia maarifa makubwa kuizidi ngome ya simba na kuandika kimiani bao hilo.
Licha ya kufungwa na Simba, KMKM imecheza soka zuri na la kufundisha na kuonesha wazi kuwa wamekomaa na wanastahili kutwaa ubingwa wa ligi ya visiwani Zanzibar.
Septemba 2 mwaka huu, Simba ilicheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar na kushinda mabao 4-3, lakini mchezo huo pia ulikuwa maalumu kuwatambulisha wachezaji wapya, Henry Joseph Shindika, Gilbert Kaze na Amisi Tambwe ambao hawakutambulishwa siku ya "Simba Day".
Lakini Henry Joseph hakucheza kufuatia kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachotarajia kushuka dimbani kesho mjini Banjul nchini Gambia, mchezo wa kukamilisha ratiba wa kuwania kufuzu fainali za kombe la Dunia huko Brazil mwakani.
Sasa Mnyama anajiandaa na mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Septemba 14 dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kikosi cha Simba SC leo: Andrew Ntalla, Haruna Shamte, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Hassan Hatibu, Kaze Gilbert, Abdulhalim Humud, Twaha Ibrahim, Said Ndemla, Amisi Tambwe, Ramadhani Chombo 'Redondo'/Betram Mombeki na Zahor Pazi.
KMKM; Mudathir Khamis, Kassim Nemshi, Faki Hamad, Iddi Mgeni, Khamis Ali, Ibrahim Khamis, Nassor Ali, Abdi Kassim 'Babbi', Ally Ahmed 'Shiboli', Mwinyi Ameir na Iddi Kambi.

Credits : Fullshangwe
Previous Post Next Post