Miss Ufilipino, Megan Young, jana aliibuka mshindi wa Miss World 2013 kwenye fainali zilizofanyika katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia ambako kulikuwa na ulinzi mkali.
“Naahidi kuwa Miss World bora zaidi,” Young mwenye miaka 23, alisema baada ya kushinda fainali hizo za 63 wakati ambapo Wafilipino kibao waliokuwa wamesafari kwenda kushuhudia fainali hizo wakisherehekea kwa kurukaruka na kupeperusha bendera ya nchi yao kwa furaha.
Licha ya kuwepo vitisho kutoka kwa kundi la Islamic Defenders Front kuwa lingeshambulia shindano hilo, polisi walisema hakuna maandamano yaliyofanyika jana. Warembo 127 walishiriki kwenye shindano hilo.
Young, aliyemrithi mshindi wa mwaka jana, Wenxia Yu wa China, alizaliwa nchini Marekani. Alipokuwa na miaka 10 alirudi kwao Ufilipino ambako ameonekana kwenye filamu na kufanya kazi kwenye TV.