KESI DHIDI YA MIZENGO PINDA KUTAJWA LEO MAHAKAMA KUU


pinda 0eabd
Kesi ya Kikatiba inayomkabili Waziri Mkuu Mizengo Pinda, leo inatarajiwa kutajwa rasmi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wakidai kuwa Pinda amevunja katiba ya nchi.
Hatua hiyo ilifuatia kauli ya Waziri Mkuu Pinda bungeni, katika mkutano wa 11 wa Bunge, kuwapa maelekezo na amri watekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
Kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013, imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, akisaidiana na Dk Fauz Twaib na Augustine Mwarija.
Tayari Mahakama Kuu imeshatoa hati ya wito kufika mahakamani leo kwa wadau wa pande zote zinazohusika katika kesi hiyo.
Mbali na Waziri Mkuu, mdaiwa mwingine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG, ambaye ni mdaiwa wa pili.
Pinda alitoa kauli hiyo inayolalamikiwa, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni, Juni 20 mwaka huu.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, aliyetaka kujua msimamo wa Serikali, kuhusu malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, kuwapiga wananchi.
"Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... Eeh, hamna namna nyingine,eeh maana lazima tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
"Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh... maana tumechoka," inasomeka hati ya madai ikimnukuu maneno ya Pinda. Katika kesi hiyo, walalamikaji,wanadai kuwa kauli hiyo ni kinyume cha katiba kwa kuwa inakiuka Ibara za 12(2) 13(1), 13(3), 13(6)(a-e).
Hivyo wanaiomba mahakama, itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha katiba na imwamuru Pinda aifute hadharani.
Wanadai kuwa kauli na amri kama hizo zinapotolewa na kiongozi mwenye hadhi kama ya mdaiwa, zinachukuliwa kama sheria inayopaswa kutekelezwa na wakala.
:CHANZO MWANANCHI.
Previous Post Next Post

Popular Items