WADHAMINI wakuu wa klabu ya Simba, Bia ya Kilimanjaro, wanatarajia kufanya mambo makubwa zaidi kwa timu hiyo katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania.
Wachezaji wa Simba wakifuatilia kwa makini semina
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa semina maalumu iliyoandaliwa na wadhamini hao kwa ajili ya wachezaji, viongozi na benchi la ufundi la Simba iliyofanyika katika Hoteli ya Kunduchi Beach jijini.
“Kila mwaka Kilimanjaro Premium Lager imekuwa ikiongeza thamani ya udhamini wake tangu tulipoanza mwaka 2008. Mwaka huu pia tutaleta kitu kingine kipya ambacho tutakitangaza wakati ukifika. Lengo ni kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika na udhamini huu,” alisema Kavishe.
Kavishe aliongeza kuwa semina hiyo ilikuwa na lengo kuelezana masuala mbalimbali yanayohusiana na udhamini na jinsi ambavyo Simba SC na Kilimanjaro Premium Lager zinanufaika kutokana na udhamini huo na kuainisha maeneo ya kuboresha.
Kwa sasa, bia ya Kilimanjaro Premium Lager hutumia takribani Sh. Milioni 495 kwa ajili ya udhamini wake kwa klabu ya Simba kila mwaka, fedha ambazo hutumika kwa ajili ya ulipaji wa mishahara ya wachezaji, ukarabati wa majengo, kugharamia Mkutano Mkuu wa Wanachama, vifaa vya timu pamoja na tamasha Siku ya Simba.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are, alisema semina hiyo imewafumbua macho viongozi na wachezaji katika masuala mbalimbali na kwamba kuanzia msimu ujao, klabu itajitahidi kufanya vizuri zaidi katika eneo la mahusiano bora na wadhamini pamoja na wadau wa klabu ya Simba.
Kwa upande wa wachezaji, Ramadhani Chomboh (Redondo), alisema semina hiyo imekuja katika wakati mwafaka kwa vile katika soka la sasa, udhamini na hadhi na maslahi ya wachezaji ni mambo yanayokwenda sambamba.
Kilimanjaro Premium Lager imefanya semina hiyo kwa klabu ya Simba ili kuboresha mahusiano yaliyopo kati ya mdhamini huyo na klabu na vile vile kuboresha. Viongozi wa klabu ya Simba pamoja na benchi la ufundi na wachezaji ambao wengi ni wapya pia walitumia fursa hiyo kuweza kukaa pamoja katika mazingira mwanana na tulivu kwenye hoteli hiyo ya kitalii huku wakishiriki michezo mbalimbali ya kujifurahisha ikiwemo mpira wa kikono, kuogelea na mingine kwa siku nzima.
Wadhamini hao wamepanga kufanya semina nyingine kama hiyo kwa ajili ya mabingwa wa ligi kuu, Young Africans SC siku zijazo.
Mwisho.
Tags:
Entertainment