MBUNGE wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan, ambaye jina lake limetajwa kuhusika na biashara haramu ya dawa za kulevya, amepata utajiri wa ghafla, akitokea kuwa teksi dereva, Raia Mwema limeelezwa.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi nchini limekuwa ‘bubu’ kuzungumzia sakata hilo la Azzan pamoja na watu wengine waliotajwa kuhusika na biashara hiyo hivi karibuni.
Azzan (48) ametumikia kwa muda wa vipindi viwili ubunge wake wa Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam, kuanzia mwaka 2005, lakini tuhuma za sasa ni mtihani mkubwa zaidi kwake kisiasa ingawa amekumbwa na masahibu mengine katika maisha yake hayo mafupi ya kisiasa.
Kwa mujibu wa mazungumzo ambayo gazeti hili limefanya na baadhi ya watu wanaomfahamu mwanasiasa huyo kwa karibu, Azzan amedaiwa kujihusisha na biashara mbalimbali, lakini zaidi ni kumiliki vyombo vya usafiri.
“Unajua kesi ya Azzan ni ya kushangaza kidogo. Miaka 20 tu iliyopita, alikuwa dereva teksi wa kawaida. Leo hii ni tajiri mzuri. Ana majumba, magari ya kifahari na ni mbunge.
“Si hali ya kawaida na pengine ndiyo maana anazua maswali mengi,” alisema mtu huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa sababu za wazi kabisa.
Kabla ya kuwa mbunge, Azzan alikuwa kiongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi waliochochea maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake mkoani Dar es Salaam.
Hata hivyo, taarifa nyingine kumhusu Azzan ni zile zinazohoji kuhusu eneo analoishi jijini.
Azzan anaishi Magomeni jirani na kituo cha kwa Bibi Paka ambako nyumba yake pengine ndiyo nzuri kuliko nyingine zote zinazomzunguka.
“Watu pia wanajiuliza, inakuwaje mbunge aishi Magomeni? Ana uwezo wa kujenga nyumba mahali popote jijini Dar es Salaam na akaishi.
“Lakini yeye ameamua kuishi Magomeni ambako ni miongoni mwa maeneo yaliyokithiri kwa biashara ya dawa za kulevya,” kilisema chanzo kingine cha habari.
Raia Mwema limeelezwa pia kwamba Azzan ametajwa kuwa na uhusiano wa karibu na waigizaji wa tasnia ya filamu na muziki wa kizazi hapa nchini- tasnia ambazo zimedaiwa kuingia kwa nguvu katika biashara hiyo katika siku za karibuni.
“Ni jambo la kawaida kuona waigiza filamu wakiigizia kwenye nyumba ya Azzan. Yaani pale kwa Iddi ni kama sebuleni kwao.
“Wanaigiza, wanakula, wanakunywa wanavyotaka. Sasa kwa sababu nao siku hizi wanakamatwa kamatwa hovyo, nadhani ndiyo maana na Azzan naye anatajwatajwa,” kinadai chanzo kingine.
Azzan alichukua ubunge wa Kinondoni mwaka 2005 kutoka kwa Peter Kabisa, na kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza katika kipindi cha kati ya mwaka 2010 hadi 2012, alikuwa mbunge wa 200 kwa uchapakazi bungeni miongoni mwa wabunge 344 waliopo bungeni.
Katika kipindi hicho bungeni, Azzan aliuliza maswali ya msingi matatu, ya nyongeza sita na akachangia katika mijadala mbalimbali mara 24.
Katika barua inayodaiwa kuandikwa na vijana wa Kitanzania ambayo imesambazwa kwa vyombo mbalimbali vya habari Tanzania kupitia mtandao wa internet kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita, Azzan na watu wengine wametajwa kuhusika na biashara hiyo.
Vijana hao wamedaiwa kusota katika jela zilizoko Hong Kong, China, kutokana na kukamatwa wakiwa na dawa za kulevya wakiwa wametokea hapa nchini.
Akizungumzia tuhuma hizo dhidi yake, Azzan amesema hahusiki na madai hayo na kwamba yuko tayari kuchunguzwa na vyombo vya dola kuhusiana na tuhuma hizo na endapo atakutwa na hatia, ataachia nafasi zake zote za uongozi alizonazo.
“Ukisoma barua iliyosambazwa mtandaoni, utaona barua yenyewe ina upungufu mwingi sana. Kwanza wenyewe hawajataja majina yao.
“Wana nini cha kuficha wakati tayari wamekamatwa? Ndiyo maana nahisi ni wapinzani wangu kisiasa wenye nia ya kutaka kunichafua.
“Tayari nimepeleka ripoti polisi. Niko tayari kuchunguzwa wakati wowote na popote. Kama nitakutwa na hatia, nihukumiwe tu kama wananchi wengine,” alisema Azzan.
Hii ni mara ya pili kwa Azzan kuingia kwenye tuhuma za kuhusika na biashara hiyo haramu kwani kwa mara ya kwanza ziliibuliwa na aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Kilumbe Ng’enda.
Ng’enda alidaiwa kutoa kauli hiyo ndani ya vikao vya ndani vya CCM katika wilaya ya Kinondoni Juni mwaka juzi, wakati Azzan alipokuwa akidai kwamba uongozi wa chama hicho mkoani Dar es Salaam unapaswa kuachia ngazi kutokana na kufanya kwake vibaya kwenye chaguzi mbalimbali.
Azzan mwenyewe alipata kutoa madai ya kutaka kuwekewa dawa za kulevya kwenye gari lake na wale aliowaita wapinzani wake wa kisiasa, na taarifa hizo alizipeleka Polisi jijini Dar es Salaam mwaka juzi.
Akichangia kuhusiana na sakata hili la Azzan, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Kabwe Zitto, alisema mbunge mwenzake huyo anatakiwa awaridhishe Watanzania kwamba hajihusishi na biashara hiyo.
Akiandika katika ukurasa wake binafsi wa Twitter, Zitto alisema, “Nimeona kuna mbunge mwenzangu ametajwa. “Nilikuwa na Idi (Azzan) kwenye mafunzo ya JKT katika kambi ya Mgambo hivi karibuni. Haonyeshi dalili za kuhusika na dawa za kulevya.
“Lakini namtaka aturidhishe kwamba hahusiki na biashara hiyo ya dawa za kulevya.
“Akubali kuchunguzwa na vyombo husika na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani,” aliandika Zitto.
Katika maelezo yake, Zitto amependekeza kwamba kila mwanasiasa nchini ambaye amewahi kutajwa kuhusika na biashara hiyo apigwe marufuku kushiriki katika siasa na pia atangazwe kuwa mtu hatari.
Alisema Watanzania wamechoka kuzika ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na kueleza kwamba kwa hali ilivyo sasa, ni wazi kwamba tatizo la dawa za kulevya ni janga la kitaifa.
Akizungumzia tuhuma hizo dhidi ya Azzan, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alimtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, ili apate taarifa zaidi.
Hata msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, aliliambia Raia Mwema kwamba atakuwa tayari kulizungumzia suala hilo pale atakapokuwa amepewa taarifa na wahusika.
Kamishina Nzowa hakuweza kupatikana hadi tunakwenda mitamboni.
Lakini kwa upande wake, Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), limesema bado halijapokea rasmi tuhuma dhidi ya Azzan na hivyo hakuna uchunguzi wowote unaofanyika dhidi yake.
Mkuu wa Interpol tawi la Tanzania, Gustav Babile, ameliambia Raia Mwema Jumanne wiki hii, kwamba ingawa tuhuma dhidi ya Azzan zimetoka nje ya nchi na linaweza kuchukuliwa kuwa ni la kimataifa, bado hana taarifa zozote kutoka nje au ndani ya nchi kuhusu suala hilo.
“Kusema ukweli sina taarifa zozote kuhusu Iddi Azzan. Hii maana yake ni kwamba taarifa zake hazijaingia katika duru za Interpol. Hilo ndilo pekee naweza kukwambia kwa sasa,” alisema.
Tags:
Social