Sababu za mastaa kubusu mikono yao

LIVERPOOL, ENGLAND
WANAFUNGA mabao kila wiki. Ni vipenzi vikubwa vya mashabiki. Lakini si mashabiki wote wanaoelewa ni kwanini wachezaji hawa huwa wanabusu viganja vya mikono yao wanapoziona nyavu za maadui wao. Wana sababu za msingi nyuma ya kitendo hiki.

Luis Suarez

Luis Suarez ukipenda unaweza kumuita Luis mabao. Anafunga kadri anavyojisikia katika msimu huu, na akifunga ni lazima abusu kiganja cha mkono wake. Katika mkono huo kuna tattoo ya mwanaye wa kike, Delfina. Suarez alijiunga na Liverpool miezi sita baada ya Delfina kuzaliwa.
Hata hivyo kwa bahati iliyoje, jina hilo la Delfina ni kinyume cha jina la Anfield ambao ni uwanja unaotumiwa na wababe hao wa Merseyside.
Mwenyewe amekaririwa akisema kwamba hakujua kuwa kinyume cha jina la mwanaye Delfina ni Anfield, lakini alikiri kwamba amevutiwa na mlinganisho huo. Mkewe Sofia aliwahi kumwambia Suarez kuwa mashabiki wa Liverpool wanasema kuwa anakibusu kiganja chake kwa sababu ya neno Anfield na si Delfina.
Alvaro Negredo

Staa mpya wa Manchester City, ambaye na yeye anatupia mabao kadri ajisikiavyo. Negredo huwa anabusu sehemu ya ndani ya kiganja chake wakati akishangilia mabao. Sehemu hiyo imeandikwa herufi C.J.R.
Herufi hizo zote zina maana yake. Herufi C inasimama kwa ajili ya mdogo wake Cesar wakati herufi R inasimama kwa ajili ya kaka yake Ruben. Herufi ya J inasimama kwa ajili ya baba yake anayeitwa Jose Maria. J hiyo hiyo pia inasimama kwa jina la mama yake anayeitwa Juana.
Alipofunga mabao matatu katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya CSKA Moscow na kuwa Mhispania wa kwanza kupiga ‘hat trick’ katika Ligi ya Mabingwa huku akiwa hachezei timu ya Hispania familia yake ilikuwepo uwanjani na Negredo daima alishangilia kwa staili hiyo.
Lengo la kubusu mkono huo wenye tattoo ni kujikumbusha kuhusu historia ya maisha yake na kuwakumbuka ndugu zake hao.
Santi Cazorla

Mmoja kati ya viungo maridadi wa Arsenal. Naye ni kati ya wachezaji ambao wakifunga wanabusu kiganja cha mkono wake.

“Siku zote nasheherekea hivyo kwa sababu mabao yangu ni zawadi kwa mwanangu. Unaweza kuona tattoo katika mkono wangu. Hiyo tattoo ni kwa ajili yake. Kama sibusu mwanangu anakasirika na nikirudi nyumbani nakuwa sina furaha.

Siku zote ni zawadi yangu kwake. Mwanangu ni kitu bora zaidi kuwahi kunitokea maishani na kila kitu ninachofanya huwa nafanya kwa ajili yake,” anasema Cazorla.

“Kuna jina lake hapa, ni Hebrew. Ni kitu kidogo cha kumpa umuhimu ninapofunga au kufanya kitu chochote.”



David Silva

Kiungo mwingine maridadi wa Hispania, David Silva anayekipiga Manchester City ni miongoni mwa mastaa ambao wanabusu viganja vyao vya mikono anapofunga mabao.

Silva ameandika jina la mtoto wa shangazi yake, Cynthia ambaye alifariki kwa ugonjwa wa saratani angali akiwa na umri wa miaka mitano tu. Kulikuwa na uvumi kwamba huenda kulikuwa na mwanamke mwingine aliyeitwa Cynthia ambaye alikuwa ni mpenzi wake, lakini baba yake Silva, Silvam Fernando Jimenez alikanusha uvumi huo.

Mara zote Silva akifunga bao anabusu kiganja chake na pia kunyoosha mikono yake miwili ikiwa ni kumbukumbu kwa Cynthia Vega Jimenez, mtoto wa shangazi yake aitwaye, Loli. Silva pia ni baba wa ubatizo wa Joana ambaye ni mtoto wa dada yake aitwaye, Cynthia.


Katika mahojiano na gazeti moja, Jimenez alimzungumzia Cynthia na kusema: “Alikufa kwa saratani. Ilimuathiri sana.
Grant Holt
Staa wa England ambaye yupo kwa mkopo katika klabu ya Aston Villa akitokea Norwich City. Kama ilivyo kwa Suarez, Silva, Cazorla na Negredo, Holt naye huwa anabusu sehemu ya juu ya kiganja chake cha mkono kila anapofunga bao.


Inadaiwa kuwa ana majina ya mke na watoto katika kiganja hicho na huwa anashangilia kwa kuwakumbuka kila anapofunga.
Wapo wanaobusu pete
Kuna wachezaji wengi wanaobusu pete pindi wanapofunga. Miongoni mwao ni mastaa wawili maarufu, Raul Gonzalez na nyota wa AS Roma, Francesco Totti.

Raul, nyota wa zamani wa Real Madrid anafanya hivyo kwa heshima ya mkewe kipenzi Mamen Sanz, aliyemuoa mwaka 1999 ambaye amemzalia watoto wanne wa kiume; Jorge, Hugo, twins Hector Mateo, pamoja na mmoja wa kike María.

Totti huwa anabusu pete yake ikiwa ni heshima kwa mkewe, Ilary Blasi ambaye alimuoa mwaka 2005 huku akimzalia watoto wawili, wa kiume Cristian na wa kike Chanel.

Totti na Blasi wanachukuliwa kama ‘Beckham na Victoria wa Italia’ na ndoa yao imekuwa ikitazamwa kwa karibu sana na waandishi wa habari
Previous Post Next Post