Dk Bilali Akutana na Raisi Mstahafu wa Iran


IMG 3354 785b3

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kiislam ya IRAN Mhe. Al-Akbar Hashemi Rafsanjani wakati Makamu wa Rais alipofika kwenye Makazi ya Rais huyo mjini Teheran Iran leo Ogast 05-2013, Makamu wa Rais yupo Nchini Iran kwa ajili ya kuhudhuria kuapishwa Rais Mpya wa Nchi hiyo alieapishwa jana jioni.


MAKAMU WA RAIS AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA KUMUAPISHA RAIS WA IRAN, 
AGOSTI 05, 2013
Makamu wa Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, jana alikuwa mmojawapo wa wageni mashuhuri katika sherehe za kumuapisha Rais wa mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Watu wa Iran Mheshimiwa Hassan Rouhani, sherehe iliyofanyika katika makao makuu ya nchi hiyo yaliyopo jijini Tehran. Kabla ya sherehe hiyo ya kuapishwa, Jumamosi Agosti 4, 2013, Mkuu wa Kidini wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei alimthibitisha Rais Rouhani na akatumia nafasi hiyo kufafanua kuhusu aina ya mahusianio ambayo Iran inataka kuyaona baina yake na nchi zingine duniani.

Mheshimiwa Makamu wa Rais alikuwa miongoni mwa viongozi wapatao 55 kutoka nchi mbalimbali walioshiriki sherehe hizi huku vyombo vya habari kutokana nchini Iran vikielezea kuwa tukio la jana kwamba ni la kihistoria kwani Iran haikuwahi kuwa na wageni mashuhuri wengi kiasi hicho katika sherehe zake za kuapisha viongozi wa nchi hiyo. Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais aliyemaliza muda wake, Rais Mahmoud Ahmadinejad.

Akihutubia wananchi wa Iran sambamba na wafutiliaji wa siasa za Iran mara tu baada ya kuapishwa, Rais Rouhani alisema Iran inategemea kuwa nchi za ulimwengu wa kwanza zitatafuta suluhu nayo kwa mazungumzo na siyo kwa kutumia vikwazo. Kauli hii alikuwa anaitoa siku moja baada ya seneti ya Marekani kupitisha kwa azimio moja vikwazo zaidi kwa Iran saa chache kabla ya Rais Rouhani kuthibitishwa na Ayatollah Khamenei, Kiongozi mkubwa kabisa na mwenye heshima ya juu katika Iran.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kimashirikiano wanaamini kuwa serikali ya Rais Rouhani ambayo aliitangaza mara tu baada ya kuapishwa, itaanza kazi kwa wakati huku ikibadili uelekeo kutoka katika siasa za mrengo wa kushoto na kuwa siasa za kawaida ambazo zitafungua mahusiano zaidi na nchi za Mashariki.

Tanzania ina uhusiano wa siku nyingi na Iran na siku kadhaa za mwisho wa utawala wa Rais Ahmadinajad, Iran ilikubali kuifutia Tanzania deni lake lililokuwepo kwa miaka mingi kwa lengo la kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili. Pia, Iran imekuwa ikisisitiza ukuzaji wa biashara hasa ya nyama kati yake na Tanzania huku kukiwa tayari na makampuni kadhaa ktoka Iran yanayowekeza katika eneo la Ujenzi.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Makamu wa Rais pia alipata fursa ya kukutana na Rais wa tatu wa Iran Akbar Hashem Rafsanjeni na kufanya naye mazungumzo kuhusu mashirikiano baina ya nchi zetu mbili. Rais Rafsanjeni aliyepata kufika Tanzania mwaka 1996 alisisitiza kuwa kuna mengi ambayo Iran ilipanga kufanya na Tanzania mbayo yalizorota baada ya utawala wake lakini ni imani yake kuwa yataendelea kufanyiwa kazi sasa. Baadhi ya maeneo aliyoyajadili ni katika elimu ambapo katika kipindi chake alianzisha kozi za Kiswahili katika vyuo vya Iran na eneo lingine likiwa la kuwezesha upatikanaji wa viwanda vya Korosho.

Kwa upande wa Mheshimiwa Makamu wa Rais alimueleza Rais Mstaafu Rafsanjeni kuwa, Tanzania inatambua uhusiano wa kihistoria iliyonao na Iran na kwamba ina nia ya dhati kuona uhusiano huo unaimarika zaidi na hasa katika maeneo ya uwekezaji na biashara za pamoja. Rais Mstaafu Rafsanjeni alisema kuwa Iran kwa sasa inakabiliwa na vikwazo kadhaa ambavyo kwa namna moja ama nyingine vimekwamisha baadhi ya mambo ambayo wao kama nchi waliyapanga kuyafanya lakini akafafanua kuwa anaona tuendako kuna nuru hivyo mafanikio ya kutimiza makubaliano baina ya nchi zetu yanaweza kufikiwa.

Msafara wa Mheshimiwa Makamu wa Rais ambao pia uliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Maalim umeondoka leo hapa Tehran kurejea nyumbani. "Tuna mengi ya kujifunza kutoka Iran na uhusiano wetu wetu una kila sababu ya kudumishwa," alimalizia Mheshimiwa Makamu wa Rais baada ya kuagana na Rais Mstaafu Rafsanjeni na saa chache kabla ya kurejea nyumbani.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Tehran, Iran
Jumatatu Agosti 05, 2013

Previous Post Next Post